
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Hosamu Hamza maarufu kwa jina la Maopena, kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi pamoja na baba yake mdogo katika tukio lililotokea eneo la Sindano, Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Julai 18, 2026, mtuhumiwa alikamatwa Julai 17, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri huko Makongo baada ya kukutwa akiwa na kisu kilichokuwa na damu pamoja na mavazi yaliyokuwa yamechafuliwa damu. Baada ya kukamatwa, alifikishwa katika kituo cha Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Polisi wamesema wakati mahojiano na mtuhumiwa yakiendelea, majira ya saa 4:00 usiku walipokea taarifa kutoka kwa wananchi kupitia Kituo cha Polisi Oysterbay kuwa watu watatu waliokuwa wanaishi katika nyumba moja eneo la Sindano, Mwananyamala, walikuwa hawaonekani huku kukiwa na damu nyingi ndani ya nyumba hiyo. Tukio hilo lilisababisha kuanza kwa uchunguzi wa kina uliowahusisha wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi.
Uchunguzi huo ulibaini kuwa watu wawili, Hamza Juma Omari maarufu Mautila (48) na Ally Juma Omari (37), ambao walikuwa miongoni mwa watu watatu waliokuwa wanaishi katika nyumba hiyo, walikuwa wameuawa na miili yao kufukiwa kwenye shimo ndani ya eneo la makazi yao.
Kwa mujibu wa Polisi, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mtuhumiwa Hosamu Hamza Juma @Maopena, ambaye ni mtoto wa marehemu Hamza Juma Omari, ndiye anayehusishwa na tukio hilo. Hata hivyo, sababu iliyomfanya kutekeleza mauaji hayo bado inaendelea kuchunguzwa.
Jeshi la Polisi limewashukuru wananchi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa ushirikiano wao katika kutoa taarifa zilizowezesha kukamatwa kwa mtuhumiwa na kuendelea kwa uchunguzi wa tukio hilo.