×

Mpenzi wa Jayden Adams Avunja Ukimya, “Hakuna Maneno ya Kuelezea Maumivu”

Mpenzi wa muda mrefu wa nyota wa soka wa Afrika Kusini, Jayden Adams, Aqueelah Adendorf, amevunja ukimya kwa kutoa salamu za majonzi kufuatia kifo cha ghafla cha mchezaji huyo aliyefariki Julai 11, 2026 akiwa na umri wa miaka 25.

Jayden Adams, ambaye alikuwa kiungo wa klabu ya Mamelodi Sundowns na timu ya taifa ya Afrika Kusini (Bafana Bafana), alifariki wiki chache tu baada ya kuiwakilisha nchi yake katika Kombe la Dunia 2026.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Aqueelah alichapisha picha mbalimbali akiwa pamoja na Adams na kueleza maumivu makubwa aliyoyapata kutokana na kumpoteza mpenzi wake.

“Hakuna maneno ya kuelezea maumivu ninayoyahisi. Pumzika kwa amani mpenzi wangu. Asante kwa kila kumbukumbu, kila kicheko, kila kumbatio na kila wakati tuliokuwa pamoja. Hukuwahi kuwa tu mpenzi wa maisha yangu, bali pia ulikuwa rafiki yangu mkubwa na mtu aliyeniunga mkono kuliko wote.”

Mpenzi wa muda mrefu wa nyota wa soka wa Afrika Kusini, Jayden Adams, Aqueelah Adendorf (kushoto) wakiwa pamoja.

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake, Aqueelah alisema:

“Sehemu ya moyo wangu imeondoka pamoja nawe, na nitaendelea kubeba upendo wako milele. Hadi tutakapokutana tena, nitakukumbuka kila siku. Pumzika kwa amani malaika wangu. Nitakupenda daima.”

Baadaye kupitia Instagram Stories, Aqueelah aliwashukuru watu wote waliomtumia salamu za pole na ujumbe wa faraja.

Alisema upendo na sapoti waliyoonyesha kwake pamoja na binti yao wa miaka mitano, Allaia-Jayda, vina maana kubwa katika kipindi hiki kigumu, huku akiomba muda kabla ya kuwajibu wote binafsi.

Kifo cha Adams kilitangazwa rasmi na Chama cha Wachezaji wa Soka Afrika Kusini (SAFPU), ambacho kilieleza kuwa kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha ghafla cha kiungo huyo.

Wiki chache kabla ya kifo chake, Aqueelah alikuwa amempongeza Adams baada ya kuitwa kwenye kikosi cha Afrika Kusini kilichoshiriki Kombe la Dunia 2026.

Katika ujumbe huo, alisema alijivunia kuona mpenzi wake akitimiza ndoto ya kuiwakilisha nchi yake, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yalitokana na juhudi, kujituma, kujitoa na imani yake kwa Mungu.

“Ulistahili kila wakati wa mafanikio haya kwa sababu nimeona namna ulivyofanya kazi kwa bidii kufikia ndoto zako. Kupitia changamoto zote hukuwahi kukata tamaa, na hilo linanifanya nijivunie kuwa kando yako na kukuunga mkono,” aliandika wakati huo.

Jayden Adams ameacha mtoto mmoja wa kike, Allaia-Jayda, ambaye alimzaa na Aqueelah mwaka 2021. Kifo chake kimeendelea kuombolezwa na familia, mashabiki, wachezaji wenzake na wadau wa soka duniani.

Leave a Comment