
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi na uhamisho wa viongozi mbalimbali katika Serikali, hatua iliyohusisha wizara, ofisi za Serikali na taasisi za umma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Jumatano Julai 22, 2026 kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rais Samia amefanya uteuzi wa Naibu Makatibu Wakuu wapya pamoja na mabadiliko ya vituo kwa baadhi ya viongozi.
Katika uteuzi huo, Dkt. Latifa Mohammed Khamis kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano.
Aidha, Prisca Burton Lwangili kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mabadiliko hayo pia yamehusisha uhamisho wa baadhi ya Naibu Makatibu Wakuu kwenda katika maeneo mengine ya Serikali. Abdallah Hassan Mitawi amehamishwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais kwenda Wizara ya Uchukuzi.
Balozi Baraka Haran Luvanda amehamishwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais kwenda Wizara ya Katiba na Sheria, huku Dkt. Franklin Jasson Rwezimula akihamishwa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kwa upande mwingine, Dkt. Maduhu Isaac Kazi amehamishwa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwenda Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ajili ya kushughulikia masuala ya Mazingira.
Katika ngazi ya taasisi za Serikali, Rais Samia amemteua Ephraim Balozi Mafuru kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), akitokea Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Uteuzi na uhamisho huo ni sehemu ya hatua za Serikali katika kuimarisha utendaji, kuongeza ufanisi na kusimamia majukumu ya taasisi mbalimbali za umma.
