×

Serikali Kuangalia Fursa Za Mikopo Kwa Wanaosoma Kozi Fupi – Waziri Mkuu

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itachunguza uwezekano wa kutoa mikopo kwa vijana wanaosoma kozi za muda mfupi katika National Institute of Transport (NIT), kufuatia ombi lililotolewa na uongozi wa chuo hicho.

Akizungumza katika Kongamano la Chama cha Wataalamu wa Lojistiki na Usafirishaji Tanzania 2026 lililofanyika NIT, Mabibo, Dar es Salaam, Julai 30, 2026, Dkt. Mwigulu alisema Mkuu wa Chuo alieleza kuwa ukosefu wa mikopo umekuwa kikwazo kwa vijana wengi kujiunga na kozi hizo, kwani wanafunzi wanaotoka kwenye familia zenye uwezo wa kifedha ndio wanaomudu gharama za masomo.

“Kozi hizi zinahitaji uwezo na utimamu wa akili, siyo uwezo wa kifedha wa familia. Serikali imepokea ombi hili na italifanyia kazi,” alisema Waziri Mkuu.

Aidha, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mpango wa Samia Scholarship, unaowapa ufadhili wanafunzi wanaofanya vizuri kitaaluma bila kujali hali zao za kiuchumi.

Pia alieleza kuwa Serikali imewekeza takribani shilingi bilioni 70 katika kuboresha miundombinu ya NIT, ikiwemo mabweni na majengo ya kufundishia, hatua inayolenga kuongeza ubora wa mafunzo yanayotolewa chuoni hapo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, alisema sekta ya uchukuzi imeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania, ikichangia takribani dola za Marekani bilioni 2.8 katika pato la taifa kwa mwaka wa fedha uliopita.

Naye Mkuu wa NIT, Dkt. Prosper Mgaya, alisema chuo hicho ni miongoni mwa vinara barani Afrika katika mafunzo ya usafirishaji na anga, kikishika nafasi ya pili Afrika baada ya Ethiopian Aviation Academy na nafasi ya kwanza Afrika Mashariki.

Aliongeza kuwa mafunzo yanayotolewa chuoni hapo tayari yamezalisha wataalamu waliopata ajira katika mashirika mbalimbali ya ndege, ikiwemo Air Tanzania Company Limited na Air Dubai, huku marubani kadhaa tayari wakihitimu na wengine wakiwa katika hatua za mwisho za mafunzo yao.

Leave a Comment