
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Crescentius Magori, amesema kikao kilichofanyika Bunju, Dar es Salaam, Agosti 2, 2026, hakikuwa Mkutano Mkuu rasmi wa klabu, hivyo maamuzi yote yaliyofikiwa hayana uhalali kisheria.
Kauli hiyo inafuatia taarifa zilizosambaa zikidai kuwa mkutano huo uliidhinisha Baraza jipya la Wadhamini wa Simba SC, baada ya wanachama waliokuwepo kuridhia majina ya wajumbe mbalimbali, akiwemo Salim Abdallah Muhene maarufu ‘Try Again’.
Hata hivyo, Magori amesisitiza kuwa mkutano huo haukuitishwa wala kuendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya Simba SC, hivyo haukuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi yoyote yanayohusu uongozi wa klabu.
Amesema kutokana na hali hiyo, hatua zote zilizodaiwa kupitishwa katika kikao hicho ni batili na haziwezi kutambuliwa na uongozi rasmi wa Simba SC kwa kuwa zinakinzana na taratibu na Katiba ya klabu.
Kauli hiyo imeongeza mvutano kuhusu uhalali wa mkutano huo na mustakabali wa maamuzi yaliyotangazwa na baadhi ya washiriki wake.
