
Madaktari wamefanikiwa kufanya upasuaji wa nadra na wa aina yake kwa mtoto ambaye alikuwa bado hajazaliwa, hatua iliyolenga kurekebisha tatizo la kuzaliwa nalo kabla ya mtoto kuja duniani.
Mtoto huyo, aitwaye Theo, alikuwa na tatizo la kiafya linalojulikana kama gastroschisis, ambapo sehemu ya utumbo hukua nje ya mwili kutokana na kutokutengenezwa vizuri kwa ukuta wa tumbo wakati wa ukuaji wa mtoto tumboni.
Mama wa Theo, Maisie Savage kutoka London, alifanyiwa upasuaji huo nchini Marekani akiwa na ujauzito wa wiki 26. Madaktari walifungua sehemu ya tumbo la uzazi na kutumia teknolojia ya kisasa ya upasuaji wa tundu dogo (keyhole surgery) kurekebisha hali ya mtoto akiwa bado tumboni.

Kwa uangalifu mkubwa, madaktari waliweza kurudisha viungo vya mtoto ndani ya tumbo lake, hatua iliyolenga kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza baada ya kuzaliwa.
Baada ya kuzaliwa, Theo ambaye sasa ana umri wa miezi mitano, anaendelea vizuri na amekuwa miongoni mwa watoto wachache duniani kufaidika na aina hiyo ya matibabu.
Madaktari wamesema Theo ni mtoto wa tatu duniani kufanyiwa utaratibu huo wa majaribio ya kimatibabu, ambao unaendelea kufanyiwa utafiti ili kusaidia watoto wengine wenye changamoto kama hiyo kabla ya kuzaliwa.
Ufanisi wa upasuaji huo umeonyesha hatua kubwa katika maendeleo ya tiba ya watoto walio na kasoro za kuzaliwa, huku wataalamu wakiendelea kutafuta njia salama zaidi za kutibu matatizo mbalimbali wakiwa bado tumboni mwa mama zao.