
Stanbic Bank Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na jamii ya Wachina nchini Tanzania baada ya kutoa udhamini wa Shilingi milioni 30 kwa Mashindano ya Mpira wa Kikapu ya Jamii ya Wachina mwaka 2026.
Katika hafla ya ufunguzi wa mashindano hayo iliyofanyika Jumamosi, Agosti 1, 2026 katika Viwanja vya Don Bosco, Namanga jijini Dar es Salaam, hundi ya udhamini ilikabidhiwa mbele ya Mgeni Rasmi pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian.
Mbali na kuwa mdhamini wa mashindano hayo, Stanbic Bank pia ilishiriki kama mshindani kupitia timu yake ya mpira wa kikapu, hatua inayoonyesha dhamira ya benki hiyo kushiriki moja kwa moja katika kujenga mahusiano na jamii.

Mkuu wa Kitengo cha Corporate & Investment Banking wa Stanbic Bank Tanzania, Ester Manase, alisema udhamini huo unaonyesha namna benki hiyo inavyoamini katika kujenga ushirikiano unaozidi huduma za kifedha.
“Kwa miaka mingi, mashindano haya yamekuwa moja ya majukwaa yetu muhimu katika kuimarisha mahusiano na jamii ya Wachina nchini Tanzania kwa sababu tunaamini kuwa ushirikiano imara hujengwa kupitia uzoefu wa pamoja, si miamala ya kifedha pekee,” alisema Manase.
Aliongeza kuwa ushiriki wa Stanbic Bank kama mdhamini na mshindani unaonyesha uhusiano wa muda mrefu na jamii ya Wachina nchini Tanzania.
“Udhamini wetu wa Shilingi milioni 30 una maana kubwa zaidi ya kugharamia mashindano. Kwa kushiriki kama mdhamini na pia mshindani, tunaonyesha kuwa ushirikiano wetu ni wa kweli na wa muda mrefu,” alisema.

Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian, aliipongeza Stanbic Bank kwa kuendelea kuunga mkono mashindano hayo, akisema michezo imekuwa sehemu muhimu ya kuimarisha urafiki na mahusiano kati ya wananchi wa Tanzania na China.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema michezo ni nyenzo muhimu ya kujenga mahusiano na kueleza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na China umeendelea kukua katika maeneo mbalimbali ikiwemo biashara, elimu, utamaduni na michezo.
Mashindano ya Mpira wa Kikapu ya Jamii ya Wachina yanaendelea kuwa jukwaa la kuunganisha wafanyabiashara, viongozi wa jamii na wadau mbalimbali, huku Stanbic Bank ikiendelea kuunga mkono mipango inayolenga kukuza mshikamano, kubadilishana tamaduni na maendeleo ya pamoja.