×

Msimu wa Pili wa EAGMA Wazinduliwa Rasmi, Safari ya Kuwatafuta Bora Yaanza

Msimu wa pili wa East Africa Gospel Music Awards (EAGMA), tuzo zinazotambua na kuthamini muziki wa injili Afrika Mashariki, umezinduliwa rasmi.

Uzinduzi huo umefanyika Agosti 1, 2026 jijini Dar es Salaam, ambapo waandaaji wamewataka wadau wa muziki wa injili kuanza kupendekeza majina ya wasanii wanaostahili kuingia katika kinyang’anyiro cha tuzo za mwaka huu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa EAGMA, Magreth Chacha, amesema mafanikio yaliyopatikana katika msimu wa kwanza yamekuwa chachu ya kufanya maboresho mbalimbali ili kuongeza ubora wa tuzo hizo.

Alisema katika msimu uliopita, wasanii wa Tanzania walifanya vizuri kwa kutwaa tuzo nyingi, jambo ambalo limeongeza matarajio na ushindani kuelekea msimu wa pili.

“Tumepata mafanikio makubwa kwa tuzo za mwaka jana. Wasanii wa Tanzania walifanikiwa kushinda tuzo nyingi, jambo ambalo linatupa wajibu mkubwa wa kuboresha zaidi tuzo hizi mwaka huu,” alisema Magreth.

Aliongeza kuwa lengo kuu la EAGMA ni kuinua hadhi ya muziki wa injili nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, pamoja na kuongeza thamani ya kazi na vipaji vya wasanii wa muziki huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa COSOTA, Victor Tesha, amesema kuendelea kwa tuzo hizo ni hatua muhimu katika kukuza na kuthamini muziki wa injili, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda haki za wasanii na kuwapa jukwaa la kutambulika kimataifa.

Msimu wa pili wa EAGMA unatarajiwa kuwaleta pamoja wasanii wa muziki wa injili kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki katika ushindani unaolenga kutambua ubunifu, vipaji na mchango wao katika tasnia ya muziki wa injili.

Leave a Comment