×

Twende Butiama Yafungasha Virago, Yaitwa Nyerere Cycling Tour

Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc kwa kushirikiana na Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA) imetangaza kubadilishwa rasmi kwa jina la msafara wa baiskeli wa Twende Butiama na kuwa Nyerere Cycling Tour, huku ikizindua mashindano mapya ya kimataifa ya mbio za baiskeli ya Vodacom Coastal Classic.

Mashindano hayo mapya ya kilomita 109 yanatarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza Jumapili, Oktoba 4, 2026, yakianza Dar es Salaam na kuelekea Makurunge mkoani Pwani kabla ya kumalizikia katika eneo la kihistoria la Old Boma, Bagamoyo.

Kwa mujibu wa waandaaji, mashindano hayo yanalenga kukuza mchezo wa baiskeli nchini na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa ya mashindano ya mchezo huo, huku yakitarajiwa kushirikisha zaidi ya waendesha baiskeli 400 kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali duniani.

Baada ya mashindano hayo, msafara wa Nyerere Cycling Tour utaanza Oktoba 5 hadi 14, 2026, ukianzia Bagamoyo hadi Butiama, mkoani Mara.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016, msafara huo umekuwa ukihusishwa na kuenzi urithi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kupitia miradi ya kuboresha mazingira ya elimu nchini.

Hadi sasa, mpango huo umefikia zaidi ya shule 107 na kuwasaidia zaidi ya wanafunzi 75,000 kupitia ujenzi wa madarasa, miundombinu ya vyoo pamoja na vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, amesema lengo la kuanzisha Vodacom Coastal Classic ni kuwapa Watanzania jukwaa la kukuza vipaji vyao na kushindana katika kiwango cha kimataifa.

“Tunataka kukuza mchezo huu. Waendesha baiskeli wengi wapo nchini, wanahitaji vifaa sahihi na mafunzo sahihi ili kufikia viwango vya kimataifa,” amesema Kamando.

Kwa upande wake, Mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour, Gabriel Landa, amesema mabadiliko hayo ya jina yanaashiria hatua mpya ya kuendeleza maono ya Mwalimu Nyerere ya usawa na fursa kwa Watanzania wote.

Leave a Comment