Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, ameipongeza kampuni ya Yas kwa ushiriki wake katika Maonesho ya Nanenane ya Mkoa wa Lindi, akisema mchango wa sekta binafsi ni muhimu katika kuharakisha maendeleo ya kilimo na mageuzi ya kidijitali nchini.
Mhe. Sangu alitoa pongezi hizo wakati alipotembelea banda la Yas katika maonesho hayo, ambapo alipokea maelezo kuhusu huduma mbalimbali za mawasiliano na huduma za kifedha kidijitali zinazotolewa na Yas pamoja na Mixx.
Amesema ushiriki wa kampuni binafsi katika maonesho kama hayo unasaidia kuwaunganisha wakulima na wananchi na fursa zinazotokana na matumizi ya teknolojia.
Kwa upande wake, Meneja wa Biashara na Masoko wa Yas – Kanda ya Pwani Kusini, Bw. George Msofe, amesema Maonesho ya Nanenane yamekuwa jukwaa muhimu la kuwafikia wananchi na kuwaelimisha kuhusu suluhisho za kidijitali zinazorahisisha mawasiliano, malipo na kukuza biashara.
“Yas itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha teknolojia na huduma za kidijitali zinawafikia Watanzania wengi zaidi, hususan wakulima, ili kuwawezesha kuongeza tija na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali,” amesema Msofe.
