×

Kikwete Atoa Tahadhari Afrika, Asema Elimu ya Kidijitali Ni Muhimu kwa Vijana – Video

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amezitaka nchi za Afrika kuongeza uwekezaji katika elimu na maendeleo ya rasilimali watu ili kuwaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi duniani.

Dkt. Kikwete ametoa wito huo baada ya kushiriki Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika, uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya mkutano huo, amesema dunia inatarajiwa kuwa na takribani ajira milioni 230 zinazohitaji ujuzi wa teknolojia za kidijitali ifikapo mwaka 2050. Kutokana na hali hiyo, amesisitiza kuwa ni muhimu kwa mataifa ya Afrika kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu yenye ubora na mafunzo ya ujuzi wa kisasa ili kuwajengea vijana uwezo wa kushindana katika soko la ajira la sasa na la baadaye.

Ameeleza kuwa maendeleo ya teknolojia yanabadilisha kwa kasi mazingira ya ajira duniani, hivyo nchi za Afrika zinapaswa kuandaa sera na mifumo itakayowezesha vijana kupata maarifa ya kidijitali, ubunifu na ujuzi unaohitajika katika uchumi wa karne ya 21.

Dkt. Kikwete amesisitiza kuwa uwekezaji katika elimu na maendeleo ya rasilimali watu ni msingi muhimu wa kuhakikisha Afrika inanufaika na fursa zinazotokana na mapinduzi ya teknolojia na uchumi wa kidijitali.

Leave a Comment