×

Netanyahu Akataa Mpango wa Trump wa Kumaliza Vita Gaza, Aweka Sharti kwa Hamas

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema Israel haikubaliani na mpango mpya wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kumaliza vita vya Gaza, licha ya Israel kupunguza kwa kiasi kikubwa mashambulizi katika eneo hilo tangu Jumatatu.

Akizungumza mbele ya Baraza lake la Mawaziri, Netanyahu alisema Israel haitakubali kuondoa wanajeshi wake Gaza hadi Hamas itakapokuwa imepokonywa silaha zote, akisisitiza kuwa baadhi ya vipengele vya mpango huo vinakubalika na vingine havikubaliki kwa Israel.

Trump anataka utekelezaji wa mpango wa vipengele 15 unaohusisha kusitishwa kwa mapigano, kuondolewa kwa wanajeshi wa Israel kwa awamu na kuanzishwa kwa kikosi cha kimataifa cha kusimamia usalama Gaza.

Kwa upande wake, Hamas imesema bado imejitolea kutekeleza mpango huo uliokubaliwa katika mazungumzo ya Cairo, lakini inamtaka Trump na wapatanishi kuhakikisha Netanyahu na serikali yake hawazuii utekelezaji wake.

Hamas imeeleza kuwa iko tayari kukabidhi silaha zake kwa ajili ya kuhifadhiwa chini ya utawala wa wataalamu wa Palestina unaoungwa mkono na Marekani, huku ikisisitiza kuwa Israel inapaswa kwanza kutekeleza ahadi zake, ikiwemo kuondoa wanajeshi na kusitisha mashambulizi.

Mjumbe wa Trump kuhusu Gaza, Nikolay Mladenov, amesema mpango huo unaendelea kujadiliwa na kwamba Israel inatarajiwa kuondoka Gaza kwa awamu, eneo kwa eneo, baada ya silaha za Hamas kuchukuliwa.

Msimamo huo wa Netanyahu unakuja wakati akikabiliwa na shinikizo la kisiasa kuelekea uchaguzi wa Israel uliopangwa kufanyika Oktoba 27, huku Mawaziri wenye misimamo mikali ndani ya Serikali yake wakipinga hatua yoyote ya kuondoka Gaza.

Waziri wa Fedha, Bezalel Smotrich, ameunga mkono msimamo wa Netanyahu akisema Israel iliingia vitani ikiwa na lengo kuu la kuiangamiza Hamas na kwamba jeshi halipaswi kuondoka hata hatua moja kutoka Gaza.

Tangu kusitishwa kwa mapigano yaliyosimamiwa na Marekani Oktoba 2025, zaidi ya watu 1,250 wameuawa katika mashambulizi ya Israel Gaza, kwa mujibu wa mamlaka za afya za Gaza, huku sehemu kubwa ya eneo hilo ikiwa chini ya udhibiti wa kijeshi wa Israel.

Leave a Comment