
LINDI: Wakulima kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara wanaotumia huduma ya Mixx kupokea malipo ya mazao yao wameanza kunufaika na zawadi mbalimbali kupitia kampeni ya ‘Vuna na Mixx’, ikiwemo pikipiki, maguta, simu janja na baiskeli.
Zawadi hizo zilikabidhiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Ayoub Mohammed Mohammed, katika hafla iliyofanyika wakati wa Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane kwenye Viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mohammed alisema matumizi ya teknolojia katika huduma za kifedha yanaendelea kuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha maisha ya wakulima, hususan katika upokeaji wa malipo ya mazao.
Alisema mifumo ya malipo ya kidijitali inaongeza usalama na uwazi katika miamala, huku ikiwapa wakulima fursa ya kupata fedha zao kwa urahisi na kutumia muda mwingi zaidi katika shughuli za uzalishaji.
“Tunapowezesha wakulima kupata malipo yao kwa njia rahisi na salama, tunawapa nafasi ya kupanga vizuri shughuli zao na kuwekeza zaidi katika uzalishaji. Ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha teknolojia inawanufaisha wananchi, wakiwemo wakulima,” alisema Mohammed.

Kwa upande wake, Mkuu wa Yas Kanda ya Pwani Kusini, Fadhila Saidi, alisema Mixx imeendelea kurahisisha upokeaji wa malipo ya mazao kwa wakulima, hususan kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghalani.
Fadhila alisema katika msimu wa kilimo wa 2025/26, zaidi ya Sh bilioni 150 zililipwa kwa wakulima kupitia Mixx, huku zaidi ya Sh bilioni 50 zikiwa tayari zimelipwa katika msimu wa 2026/27.
“Lengo ni kuhakikisha mkulima anapokea fedha zake kwa haraka, salama na kwa uwazi. Zawadi tunazotoa pia zina matumizi ya moja kwa moja katika shughuli zao; kwa mfano, guta na pikipiki zinaweza kuwasaidia katika usafirishaji wa mazao na shughuli nyingine za kila siku,” alisema Fadhila.
Katika hafla hiyo, jumla ya maguta manne, pikipiki tano, simu janja sita pamoja na baiskeli zilikabidhiwa kwa baadhi ya wakulima, ikiwa ni sehemu ya zawadi za kampeni ya ‘Vuna na Mixx’ kwa waliotumia huduma hizo katika msimu uliopita.
Mbali na kupokea malipo ya mazao, Fadhila alisema wakulima wanaweza kutumia huduma ya Kilimo Pesa kupata mikopo kwa ajili ya shughuli za kilimo. Pia kuna huduma ya Afya Mkulima, inayowawezesha wakulima kupata bima ya afya kwao na familia zao.
Baadhi ya wakulima waliopokea zawadi hizo, akiwemo Mohammed Chikawe, Hassani Mohammed na Issa Mtiko, walisema zawadi hizo zimewapa hamasa ya kuendelea kutumia huduma za kifedha za kidijitali katika kupokea na kusimamia mapato yatokanayo na shughuli zao za kilimo.
Walisema matumizi ya malipo ya kidijitali yamewarahisishia kupata fedha zao bila kulazimika kusafiri umbali mrefu au kubeba fedha taslimu, jambo walilosema linaongeza usalama na ufanisi katika