×

Mainstream Group Yang’ara Tehama Awards 2026, Yanyakua Tuzo Mbili

DAR ES SALAAM: Kampuni ya Mainstream Group Limited imeendelea kung’ara katika sekta ya teknolojia nchini Tanzania baada ya kushinda tuzo mbili katika Tuzo za Tehama Awards 2026 zilizofanyika jijini Dar es Salaam.

Kampuni hiyo ilishika nafasi ya pili katika kipengele cha Ubunifu wa Teknolojia katika Mifumo ya Malipo, huku Mkurugenzi wake, Deogratius Lazari Mosha, akitambuliwa miongoni mwa viongozi wanaofanya vizuri katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Tuzo hizo zilitolewa usiku wa Agosti 9, 2026, katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Johari Rotana, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa teknolojia na uchumi wa kidijitali.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Angela Kairuki.

Katika kipengele cha Ubunifu wa Teknolojia katika Mifumo ya Malipo, Mainstream Group ilifanikiwa kushika nafasi ya pili baada ya kushindanishwa na taasisi mbalimbali, ikiwemo NMB Bank.

Tuzo hiyo inalenga kutambua taasisi zinazotumia teknolojia kwa ubunifu katika kuboresha, kurahisisha na kuongeza ufanisi wa huduma za kifedha.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Mainstream Group, Deogratius Lazari Mosha, ametambuliwa kutokana na mchango wake katika kukuza na kuendeleza teknolojia nchini.

Mosha si mgeni katika tuzo za kimataifa, kwani mwaka 2024 aliwahi kutunukiwa tuzo ya Kiongozi Bora katika Ubunifu Barani Afrika kupitia Forty Under 40 Africa Awards, zilizoandaliwa na Xodus Communications Limited.

Ushindi wa mwaka huu unaifanya Mainstream Group kutambuliwa kwa mara ya pili katika Tuzo za Tehama nchini Tanzania. Mwaka 2024, kampuni hiyo ilishinda tuzo katika kipengele cha Ubunifu katika Matumizi ya TEHAMA kwenye Sekta ya Fedha.

MCHANGO KATIKA SEKTA MBALIMBALI

Mafanikio hayo yamekuja miezi kadhaa baada ya Mainstream Group kushinda zabuni ya kutengeneza mfumo wa usajili wa wanachama wa Simba Sports Club, mfumo unaolenga kurahisisha mchakato wa usajili wa wanachama pamoja na utoaji wa kadi zao.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mainstream Group, Pascal William, amesema kutambuliwa kwa kampuni hiyo kunatoa msukumo zaidi wa kuendelea kuwekeza katika ubunifu na kutengeneza mifumo inayolenga kutatua changamoto katika sekta mbalimbali.

William amesema Mainstream Group imekuwa ikishiriki katika kutengeneza mifumo inayorahisisha huduma za kibenki pamoja na mifumo ya elimu kwa vyuo vikuu, ikiwemo Smarti Uni.

Amesema uwekezaji huo katika teknolojia umekuwa na mchango pia katika kuibua fursa za ajira kwa vijana nchini.

Kwa mujibu wa William, Mainstream Group kwa sasa inatoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa zaidi ya vijana 100 nchini, huku kampuni hiyo ikiendelea kuchangia mapato ya Serikali kupitia ulipaji wa kodi.

Ushindi wa tuzo hizo mbili unaongeza nguvu katika jitihada za Mainstream Group za kuendeleza ubunifu wa kiteknolojia na kutengeneza suluhisho za kidijitali zinazolenga kuboresha huduma na maisha ya Watanzania.

Leave a Comment