ILIPOISHIA KWENYE GAZETI LA IJUMAA:
“Najua unataka kujua kama ni vinyama kwa maana gani! Ni vinyama kwa maana ni vidogo sana, vidogo kama panya buku, lakini wanaishi juu ya maji na wanatembea juu ya maji. Hivi meli inavyotembea, vinapisha kwa ubishi. Macho yao ni makali sana ndiyo maana unaona hali ya kumetameta kama hivi.
SASA ENDELEA…
Sasa si unaona hatuoni tena vitu vya kumetameta? Meli imeingia kwenye lile eneo nililokwambia ni la giza nene,” aliniambia Nurdin huku akinigeukia lakini hatukuweza kuonana vizuri kwa sababu ya giza totoro.
Ni kweli vile vimetameta sikuviona tena, lakini nilimuuliza Nurdin amejuaje tuko kwenye giza totoro wakati ni usiku na katikati ya bahari kutoka Sri Lanka kwenda Sumtra, akajibu:
“Angalia juu.”
Niliangalia juu lakini sikuona kitu, akaniuliza:
“Unaona nini?”
“Sijaona kitu.”
“Hata nyota angani?” aliniuliza.
“Sijaona hata nyota angani. Kwani zimekwenda wapi?”
“Ndiyo maana nimesema tunapita kwenye kiza kinene lakini sasa angalia tena juu halafu niambie unaona nini?”
Niliangalia juu tena nikaona nyota nyingi, nikamwambia:
“Naona kama nyotanyota vile au wewe Nurdin unaona nini kwa kutumia macho yako?”
“Oke na mimi nakiona unachokiona wewe, hii inaashiria kwamba, sasa tumetoka kwenye lile giza. Ni giza ambalo linashangaza wengi, kwani hata tutakaporudi kama itakuwa mchana, tutakutana nalo.
“Halafu kulipita kwake ni dakika tano tu, mnatokea kwingine. Lakini lile giza linasadikiwa kuwa ndiyo kwenye mlango mkuu wa kuingilia katika makazi ya kuzimu,” Nurdin aliniambia huku akinishika mkono.
Nilitetemeka sana, nikamwomba Nurdin tushuke kuingia kwenye viti vya ndani, tukashuka.
Safari ilikuwa ikiendelea, sisi tulikuwa tumekaa, Nurdin akaniambia:
“Bwana Tolu, baharini kuna mambo mengi sana. Unaweza kuamua kuacha kazi. Hata hivyo, tukirudi itabadi nikupeleke mahali kwa ajili ya kuwekwa sawa. Wewe ni mwepesi sana. Kwa hiyo huwezi kufanya hii kazi ya kutembea kwenye maji wakati mwingi.”
Wakati anaongea hivyo, mimi nilikuwa nikimwangalia tu, mara akaangalia kwenye dirisha moja lililokuwa kisogoni kwangu, akasema:
“Mfano hebu geuka uangalie pale juu.”
Niligeuka kwa woga, nikaangalia, nikamwona mrembo mweupe sana akituangalia kwa tababamu kisha akapungia mkono kama anayetuaga halafu ghafla akapotea machoni petu.
“Unamfahamu?” nilimuuliza Nurdin.
“Bwana Tolu, unadhani naweza kumfahamu? Kwanza hujajiuliza huko nje ya meli amesimamaje wakati hakuna sehemu ya kusimama?” Nurdin aliniuliza.
Nilimuuliza kama kweli hamjui yule mrembo, akasema: “Yule ni jini bwana tolu! Huku baharini kuona majini ni jambo la kawaida sana.”
Ghafla meli ikatikisika yote, nikashtuka, Nurdin akaniambia:
“Eneo hilo sijui lina nini chini, lakini kila tukipita lazima meli itikisike. Kuna wenyeji huko tunakokwenda waliwahi kusema, chini ya bahari eneo hilo kuna meli iliwahi kuzama miaka mingi iliyopita na ilikuwa na abiria wengi, lakini hakuna aliyepona. Ndiyo sasa maajabu yake ni hayo.
“Lakini pia huko mbele tunakokwenda tutafika mahali utasikia kelele za watu, kama wanaomba msaada.”
Kabla Nurdin hajamaliza kusema, zikasikika kelele nyingi sana, zilikuwa za watu wanaolalamikia kitu au kutaka kuokolewa katika hatari.
“Ndiyo hizo?” nilimuuliza Nurdin.
Zilikuwa kelele za kutikisa anga. We angalia tulikuwa ndani ya meli lakini kelele zilifika hadi ndani na ikasikika kama waliopiga kelele wamo humohumo ndani ya meli yetu.
Nurdin alisema kuwa, hizo kelele zinasadikiwa ni za watu waliowahi kuzama na meli, pia miaka mingi iliyopita na walikuwa kwenye chumba kimoja. Sasa inasadikika kwamba, walichukuliwa kimiujiza na viumbe wa baharini.
Kwa hiyo tangu wameingia humo wanapiga kelele kila siku ya Mungu na wakati mwingine huwa wanalia sana.
“Nurdin inawezekana hizo kelele wanapiga muda wote au kuna wakati wanapumzika?”
“Sijui, lakini wanasema kwamba, wanaposikia meli au mlio wa ndege ndiyo huanza kupiga kelele. Nasikia wachungaji na mashehe walishajaribu kufika eneo hili kwa lengo wa kuwaokoa hawa watu lakini walipata misukosuko mikubwa wakashindwa kufanikisha.
“Ndugu wa waathirika wameshakuja na kuzitambua sauti za wapendwa wao kwani nao huwataja kwa majina wale wanaowafahamu lakini ndiyo hivyo tena,” Nurdin aliniambia tukiwa tumeshalipita eneo hilo.
Maneno hayo kwangu yalikuwa mageni sana, kweli moyoni nikaanza kuona ugumu wa kazi ya ubaharia ambayo nilikuwa naipenda sana tangu nikiwa mdogo.
“Bwana Tolu,” aliniita Nurdin.
“Naam,” niliitika nikijua anataka kuniambia kitu kingine.
Je, unajua kilichoendelea? Usikose kusoma mwendezo wa mkasa huu wa kusisimua kesho kwenye Gazeti la Ijumaa.