Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Tabu alipomwambia Dorcas kuhusu tabia ya ukali ya mama Bite. Je, kilifuatia nini? Songa mbele…
Tabu aliniambia kuwa pale kwa mama Bite alikuwa anavumilia mengi kwa sababu alikuwa mkali hata kwa mambo yasiyostahili na kuna wakati alipokesea jambo alikuwa akimchapa na kumtukana.
Aliponiambia hivyo na jinsi nilivyomuona mama huyo, nilimwuliza kama aliyoyasema yalikuwa yana ukweli akaniambia kweli lakini sikuamini na kuhisi Tabu alikuwa na matatizo tu!
“Mama mwenye moyo wa upendo namna ile aliyeamua kunichukua na kuahidi kunisomesha awe na roho mbaya kama anavyosema huyu Tabu, sidhani hawezi bwana!” nilijisemea moyoni.
Kule mashineni tulizungumza mengi lakini moyoni niliamini mama Bite alikuwa mama mzuri sana na kuhisi Tabu alikuwa na mambo yake yaliyomfanya mama huyo kumuadhibu kama alivyoniambia.
Umeme uliporudi tulisaga na kurejea nyumbani, tulipofika mama alimwuliza Tabu tulichelewa wapi, akamwambia hakukuwa na umeme.
“Eti Dorcas mmechelewa kwa sababu hakukuwa na umeme au huyu mwenyeji wako alikuwa kwa wanaume zake, sema ukweli?” mama aliniuliza.
Licha ya kumwambia umeme haukuwepo tuliamua kusubiri mama hakuelewa, alisema alinifundisha niseme uongo kwa sababu pale nyumbani palikuwa na umeme.
Bila kufahamu kwamba eneo tulilokuwepo ilitokea hitilafu ya umeme, mama alimdaka Tabu na kuingia naye ndani, akaanza kumtandika huku akisema hataki wasichana malaya katika nyumba yake.
Licha ya Tabu kulia na kumwambia mama hakuwa kwa wanaume aamini maneno yetu hakumwelewa, alimtandika hadi fimbo aliyokuwa akiitumia ikawa vipande.
“Dorcas, kwa kuwa nimeamua kuishi na wewe hapa sitaki uige mambo ya umalaya kama anayoyafanya huyu kinyago, anakufundisha uongo na wewe unakubali, mimi sitaki mambo ya ujinga na upuuzi,” Dorcas anasema mama Bite alimwambia.
Aliongeza kuwa hataona shida kunifukuza nyumbani kwake licha ya kuniahidi kunisomesha na kwamba hakutaka tuwafundishe watoto wake tabia mbaya.
Baada ya mama kumpa kichapo Tabu, alimwambia tukaendelee na kazi, japo wakati huo hatukuwa na kazi ikabidi tutafute cha kufanya,Tabu akaenda chumbani na kutoa nguo za akina Bite tukaanza kuzifua.
Wakati tunafanya kazi hiyo, Tabu alikosa raha akawa anatiririkwa machozi kufuatia kitendo cha mama kumuadhibu bila kosa.
Nilimsihi awe na amani na avumilie lakini akaendelea kulia na kuniambia alikuwa amemvumilia sana mama na kufikia tamati na kwamba hata kama kwao walikuwa maskini atarudi huko kuliko kuendelea kuteseka.
Maneno ya Tabu yalinihuzunisha sana kwani alichokiongea kilikuwa kweli tupu, hata hivyo nilimsihi asiwe na hasira akaniambia alichoshwa na manyanyaso.
Siku hiyo Tabu alishinda akiwa mnyonge, tukiwa chumbani kwetu alifungua begi lake akatoa baadhi ya nguo zilizokuwa zinambana akanipatia kwa vile sikuwa na nguo nyingi.
Hakuishia hapo, alinipatia jozi mbili za viatu, nilifurahi sana kwa upendo wake. Jioni ilipofika mimi na akina Bite tulikaa nje tukawa tunapiga stori na kumuacha Tabu chumbani.
Nyumba tuliyokuwa tunaishi ilikuwa na milango miwili mmoja wa kuingia nyumba kubwa na wa uani, wakati tunazungumza Tabu alitoka kwa kupitia mlango wa uani na kutoweka.
Aliyekuwa wa kwanza kubaini Tabu hakuwepo pale nyumbani alikuwa Bite, kwani chumbani kwetu hakukuwa na begi na vitu vyake vingine.
Tulipobaini hakuwepo tulitoka na kuwauliza majirani ndipo mama mmoja alisema alimuona akiwa kabeba begi na mfuko wa rambo na alipomuuliza alikuwa akienda wapi alimwambia lilikuwa begi la mgeni wetu.
Kufuatia Tabu kutoroka, mama aliingia chumbani na kuuliza kama hakuchukua vitu visivyomhusu, ulipofanyika ukaguzi kila kitu kilikuwepo kasoro begi lake na vitu vyake.
Bite alipoangalia ndani ya begi langu alikuta zile nguo nilizopewa na Tabu na viatu vilivyokuwa uvungu wa kitanda, akaniuliza nani aliziweka nikamwambia alikuwa amenipatia, akaenda kumwambia mama.
Mama aliingia chumbani na kuniuliza kuhusu nguo hizo nikamwambia nilipewa na Tabu, akaanza kunishambulia kwamba nilikuwa najua mpango wake wa kutoroka akanizaba kibao cha nguvu nikaangukia kitandani.
Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni tumia namba iliyopo hapo juu