×

Video: Chalamila Atoa Siku Saba Kwa Mabasi Kurejea Magufuli Stendi

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa siku saba kuanzia leo, Agosti 11, 2026, kwa mabasi yote yanayoegeshwa katika eneo la Shekilango kuhamishia shughuli zao katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Magufuli.

Akizungumza na vyombo vya habari, Chalamila amesema madereva na wamiliki wa mabasi ya mikoani wanapaswa kuhakikisha mabasi yao yanarejea katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Magufuli ndani ya muda uliotolewa.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano wa magari pamoja na kuondoa kero zinazoweza kujitokeza kutokana na mabasi kuendelea kutumia maeneo ambayo hayajatengwa rasmi kwa ajili ya shughuli za usafirishaji.

Kwa mujibu wa Chalamila, zoezi hilo limeanza leo, Agosti 11, na linatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 17, 2026.

Aidha, amewataka wamiliki, madereva na wahusika wengine katika shughuli hizo kuhakikisha wanakuwa na vibali pamoja na nyaraka muhimu za utambulisho ili kurahisisha utekelezaji wa agizo hilo.

Chalamila amesisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuweka utaratibu mzuri wa usafirishaji na kuhakikisha maeneo ya barabara na vituo visivyotengwa rasmi yanaondolewa matumizi ya mabasi ya mikoani.

Na Lailath Burhan

Leave a Comment