×

Rais Samia Awapongeza Wazanzibar Kwa Kudumisha Amani, Afananisha Siasa Na Simba Na Yanga (Picha +Video)


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuonesha ukomavu wa kisiasa na kudumisha amani wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na wananchi wakati akipita kwenye mitaa mbalimbali ya Mji Mkongwe (Stone Town), Zanzibar, tarehe 10 Agosti, 2026.

Akizungumza leo, Agosti 11, 2026, na wananchi pamoja na wanachama wa CCM katika eneo la Kisonge, Zanzibar, Dkt. Samia amesema Zanzibar imepiga hatua katika masuala ya kisiasa, akieleza kuwa uchaguzi huo ulifanyika kwa amani bila kutokea vitendo vya uvunjifu wa amani au watu kuumizwa.

Rais Samia amesema ushindani wa kisiasa haupaswi kuwa chanzo cha uhasama miongoni mwa wananchi, akifananisha hali hiyo na ushindani wa klabu kongwe za soka nchini, Simba na Yanga.

“Nawapongeza na saluti Wazanzibari mwaka huu. Tumefanya uchaguzi hakuna aliyenyukuliwa… Tumekwenda tumefanya kwa amani na utulivu… sisi wote ni wa nchi hii, wa visiwa hivi na lazima tuishi pamoja kwa maendeleo yetu. Kwa hiyo kushindana kumo, hata Simba na Yanga si wanashindana,” amesema Dkt. Samia.

Aidha, Rais Samia amewataka wananchi wa Zanzibar kutumia fursa zinazotokana na mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji yanayowekwa na Serikali, ili kuongeza kipato na kuchochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja pamoja na jamii kwa ujumla.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akifurahia nyimbo mbalimbali za Taarabu asilia baada ya kuwasili katika eneo la Jaws Corner katikati ya Mji Mkongwe (Stone Town), Zanzibar tarehe 10 Agosti, 2026.

Amesisitiza kuwa kulinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar si suala la kupiga kura pekee, bali pia ni kushiriki kikamilifu katika shughuli na miradi ya maendeleo.

Vilevile, amewataka Wazanzibari kuendelea kudumisha upendo, mshikamano na amani, akieleza kuwa mazingira hayo ni muhimu katika kuvutia watalii na wawekezaji zaidi na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.

Rais Samia akiwa kwenye picha na vijana wa Makachu pembezoni mwa bustani ya Forodhani, Zanzibar tarehe 10 Agosti, 2026.

Leave a Comment