
Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amesema timu yake iko tayari kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, huku akieleza matarajio yake kuelekea Kariakoo Derby yake ya kwanza tangu alipokabidhiwa jukumu la kuiongoza klabu hiyo.
Mngqithi ameyasema hayo leo, Agosti 11, 2026, mjini Zanzibar, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo utakaochezwa kesho, Agosti 12, katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Kocha huyo amesema maandalizi ya Yanga yamekwenda vizuri licha ya timu kuwa na muda mfupi wa kujiandaa kutokana na michezo iliyochezwa mwishoni mwa wiki.
Amesema hali hiyo pia imeikumba Simba, hivyo anaamini timu zote zimeingia katika mchezo huo zikiwa katika mazingira yanayofanana ya maandalizi.
“Habari za asubuhi kwa wote. Hii ni mara yangu ya kwanza kushiriki katika Derby hii, hivyo nina hamu kubwa ya kuona kitakachotokea,” amesema Mngqithi.

Ameongeza “Maandalizi yetu yamekwenda vizuri, ingawa hatukupata muda mrefu wa kujiandaa kwa sababu timu zote mbili zilikuwa na michezo mwishoni mwa wiki. Pia hatukupata muda wa kutosha wa maandalizi wakati wa kipindi cha kabla ya msimu kuanza. Hata hivyo, naamini hali hiyo ni sawa pia kwa Simba.”
Mngqithi amesema ana imani kubwa na kikosi chake, akieleza kuwa kina wachezaji wenye uwezo wa kucheza soka zuri na kuvutia.
“Kwa hiyo itakuwa jambo la kuvutia kuona namna timu zote mbili zitakavyocheza. Nina imani kubwa na timu yangu. Tuna kikosi chenye uwezo wa kucheza soka zuri na la kuvutia,” amesema.
Amesema kikosi hicho kina uwezo wa kutoa nguvu na ubora unaohitajika ili Yanga iweze kucheza vizuri na kudumu katika kiwango kizuri kwa muda wote wa mchezo.
“Zaidi ya kutaka kushinda mechi, mimi ni kocha ninayependa sana soka zuri. Nataka kucheza aina ya soka ambayo itawafanya watu wawe na sababu ya kuacha shughuli zao, kutoka majumbani kwao na kuja uwanjani kutazama timu yao ikicheza,” amesema.
Akizungumzia Simba, Mngqithi amesema anatambua mwenendo mzuri wa wapinzani wao na anawaheshimu kutokana na ubora waliouonesha.
“Ni kweli wapinzani wetu wamekuwa na mwenendo mzuri, lakini naamini kuna baadhi ya tofauti kubwa ambazo nimeziona katika namna wanavyocheza. Lakini kwa ujumla tunawaheshimu na tunatambua ubora wao,” amesema.
Hata hivyo, amesema Yanga haijaenda Zanzibar kwa ajili ya kushiriki tu, bali ina lengo la kushindana na kutoa changamoto kubwa kwa Simba.
“Naweza kuwaahidi mashabiki wetu kwamba hatukuja hapa kwa ajili ya kushiriki, tumekuja hapa kushindana na kuwapa Simba changamoto kubwa na lengo letu ni kuhakikisha tunafanya vizuri na kulitetea taji hili,” amesema Mngqithi.
Wakati huo huo, Yanga imewataka mashabiki wake kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa New Amaan Complex kesho na kuisapoti timu katika kila dakika ya mchezo.
“Tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi uwanjani kesho, watusapoti na kuwa nyuma yetu katika kila dakika ya mchezo. Tunajua uwezo mkubwa wa kushangilia wa mashabiki wetu na tunahitaji sapoti yao ili kutupa nguvu zaidi ya kupambana hadi dakika ya mwisho,” amesema Mohamed Hussein.
Mchezo huo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga utachezwa kesho, Agosti 12, 2026, katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kuanzia saa 2:30 usiku.
Stori na Kija Z Enock | GPL