Mshambuliaji Selemani Mwalimu ‘Gomez’ leo, Agosti 11, 2026, amewasili Visiwani Zanzibar akiwa pamoja na Ali Kamwe na muda mfupi baadaye ameanza mazoezi na timu yake mpya ya Yanga.
Gomez, ambaye ni miongoni mwa wachezaji wapya walioungana na kikosi hicho, ameanza rasmi maandalizi yake akiwa Zanzibar kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.
Kupitia ukurasa wake rasmi, Yanga imeweka picha za mshambuliaji huyo akiwa katika mazoezi na wachezaji wenzake, huku ikitumia ujumbe mfupi unaoashiria kuanza kwa majukumu yake mapya ndani ya klabu hiyo.

“Hakuna muda wa kupoteza, kazini,” Yanga imeandika kwenye chapisho hilo likiambatana na picha za Gomez akiwa mazoezini.
Kuwasili kwa Gomez na kuanza mazoezi kunakuja wakati Yanga ikiendelea na maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, unaotarajiwa kuchezwa kesho, Agosti 12, 2026, katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.



