BANDAR SERI BEGAWAN: Sultan wa Brunei, Hassanal Bolkiah, amemvua mkwe wake, Pengiran Raabi’atul Adawiyyah, vyeo vyake vya kifalme akidaiwa kuonyesha tabia isiyofaa na kukosa heshima kwa familia ya kifalme.
Pengiran Raabi’atul Adawiyyah, mwenye umri wa miaka 33, alijiunga na familia ya kifalme ya Brunei mwaka 2015 baada ya kufunga ndoa na Prince Abdul Malik, mtoto wa pili wa Sultan Bolkiah kutoka kwenye ndoa yake ya kwanza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Grand Chamberlain, hatua hiyo imechukuliwa baada ya mwenendo wa Pengiran kutathminiwa kuwa haufai kwa mwenza wa mwanafamilia ya kifalme.
Taarifa hiyo pia ilisema vitendo vyake vilionekana kuchafua jina la ufalme na kuonyesha ukosefu wa heshima kwa Sultan Hassanal Bolkiah.
Hata hivyo, ikulu haijaeleza wazi ni kitendo gani hasa kilichosababisha kuvuliwa kwa vyeo hivyo.

Pengiran na Prince Abdul Malik wamejaliwa watoto wanne, ambao ni Princess Muthee’ah, mwenye miaka 10, Princess Fathiyyah, miaka minane, Princess Khaalishah, miaka sita, na Princess Nabeelah, mwenye miezi 16. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vyeo vya watoto hao havijaathiriwa na uamuzi huo.
Sultan Hassanal Bolkiah, mwenye umri wa miaka 80, ni miongoni mwa watawala waliodumu muda mrefu zaidi duniani. Mbali na kuwa Sultan wa Brunei, pia ni Waziri Mkuu wa nchi hiyo tangu ilipopata uhuru kutoka Uingereza mwaka 1984.
Brunei ina mfumo wa utawala unaompa Sultan mamlaka makubwa ya kiutendaji, huku Bolkiah pia akiwa anashikilia nyadhifa za Waziri wa Ulinzi, Waziri wa Mambo ya Nje na Waziri wa Fedha.
Utawala wake umekuwa ukikosolewa mara kwa mara na mashirika ya haki za binadamu kutokana na sheria kali zinazotokana na tafsiri ya sheria za Kiislamu.
Mwaka 2014, Sultan Bolkiah alisukuma utekelezaji wa hatua mbalimbali za sheria ya Sharia nchini Brunei, ikiwa ni pamoja na adhabu kali kwa baadhi ya makosa.
Mwaka 2019, Brunei ilianza kutekeleza kifungu cha sheria kinachotaja adhabu ya kifo kwa baadhi ya makosa, ikiwemo ngono ya jinsia moja na uzinzi, ingawa utekelezaji wa adhabu hiyo haujaripotiwa kutumika.
Hatua hiyo ilizua ukosoaji mkubwa wa kimataifa, huku baadhi ya watu mashuhuri akiwemo George Clooney na Elton John wakitoa wito wa kususiwa kwa hoteli zinazohusishwa na Sultan.
Kwa sasa, hatua ya kumvua Pengiran Raabi’atul Adawiyyah vyeo vya kifalme imeongeza mjadala kuhusu taratibu, nidhamu na mamlaka ndani ya familia ya kifalme ya Brunei.
