Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imeshindwa kuendelea leo Ijumaa, Agosti 14, 2026, baada ya shahidi wa 18 wa upande wa mashtaka kudaiwa kupata dharura ya kiafya na kushindwa kufika mahakamani.
Upande wa Jamhuri uliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo, ukieleza kuwa shahidi huyo amepata changamoto ya kiafya na amelazimika kwenda hospitalini.
Hata hivyo, Lissu alipinga ombi hilo, akirejea amri iliyowahi kutolewa na mahakama kwamba upande wa mashtaka unatakiwa kuwasilisha mashahidi wasiopungua wawili kwa siku wakati kesi inapokuwa ikiendelea.
Lissu aliiomba mahakama kutokubali ombi la Jamhuri, akisema yuko tayari kesi hiyo iendelee siku hiyo na upande wa mashtaka ulete mashahidi wengine.
Aidha, Lissu amesema iwapo Jamhuri imeshindwa kuendelea na ushahidi, basi inapaswa kufunga ushahidi wake na kesi hiyo kuingia katika hatua inayofuata.
Katika msimamo wake, Lissu alidai kuwa upande wa mashtaka “umekata pumzi” na hivyo hakuna sababu ya kuendelea kuahirisha mwenendo wa kesi.
Hata hivyo, Jopo la Majaji watatu linalosikiliza kesi hiyo limekubali ombi la upande wa Jamhuri na kuahirisha shauri hilo.
Jopo hilo linaongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiana na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.
Kwa uamuzi huo, kesi hiyo inatarajiwa kuendelea Jumatatu, Agosti 17, 2026, ambapo upande wa Jamhuri unatarajiwa kuwasilisha mashahidi wake waliobaki.
