×

Jamhuri Yafunga Rasmi Ushahidi Katika Kesi ya Uhaini ya Tundu Lissu

Upande wa Jamhuri umefunga rasmi ushahidi wake katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, baada ya kuwasilisha mahakamani mashahidi 17 kati ya 30 waliokuwa wameorodheshwa.

Hatua hiyo imechukuliwa leo, Agosti 17, 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambako kesi hiyo iliendelea mbele ya Jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.

Majira ya saa nne asubuhi, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, aliwasilisha taarifa ya maombi ya upande wa Jamhuri ya kufunga ushahidi, akieleza kuwa ushahidi uliotolewa na mashahidi waliokwisha kutoa ushahidi mahakamani unatosha kuthibitisha hoja za upande wa mashtaka.

Katuga alisema baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa mahakamani pamoja na mashahidi waliokuwa bado hawajatoa ushahidi, upande wa Jamhuri ulifikia uamuzi kwamba hauoni umuhimu wa kuendelea kuwasilisha ushahidi zaidi.

“Upande wa Jamhuri baada ya kupitia ushahidi ambao tayari umewasilishwa mahakamani na kuangalia ushahidi uliobakiwa, tumeuchambua na kuangalia hoja zilizokubaliwa upande wa Jamhuri, ukajikuta kwamba unaona ushahidi ambao tayari umeshautoa ni ushahidi toshelezi,” alisema Katuga.

Aliongeza kuwa kuendelea kuleta ushahidi zaidi kwa lengo la kuthibitisha hoja ambazo zilikubaliwa wakati wa usikilizwaji wa awali wa kesi (Preliminary Hearing) kungekuwa kinyume cha sheria.

“Hivyo basi tunafurahishwa kuitaarifu mahakama hii tukufu kwamba upande wa Jamhuri umefunga ushahidi wake kwa mashahidi hao 17,” aliongeza Katuga.

Kwa upande wake, Tundu Lissu aliiambia mahakama kuwa hakuwa na pingamizi na uamuzi huo wa upande wa Jamhuri.

Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, Jopo la Majaji lilikubaliana na hoja hiyo na hivyo ushahidi wa upande wa Jamhuri ukafungwa rasmi.

Awali, upande wa Jamhuri ulikuwa umeorodhesha jumla ya mashahidi 30, lakini ulieleza kuwa haukuwa na ulazima wa kuwaita wote mahakamani na ungeweza kutumia idadi ya mashahidi ambao ungeona wanatosha kuthibitisha mashtaka yake.

Lissu: Baada ya kusikiliza ushahidi wao na mashahidi wao 17, naomba kutoa hoja kwenu, Waheshimiwa Majaji, kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kabisa kuthibitisha kwamba kuna kesi ya uhalifu inayoweza kuiwezesha Mahakama hii kumtaka mshtakiwa ajitetee.

Kesi hiyo inaendelea mahakamani, huku hatua zinazofuata zikisubiriwa baada ya upande wa Jamhuri kufunga rasmi ushahidi wake.

Leave a Comment