
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Iran haitafanya makubaliano anayoyaona kuwa muhimu ili kumaliza vita kati ya Marekani na Iran, huku mazungumzo kati ya pande hizo yakiendelea kukwama.
Akizungumza Jumatatu katika Ofisi ya Oval, Trump alisema Marekani inaingia katika mzozo huo kwa sababu moja kuu kuhakikisha Iran haipati silaha za nyuklia.
“Hawatafanya aina ya makubaliano ninayoona ni muhimu,” Trump alisema, akisisitiza kuwa Iran “haiwezi kuwa na silaha ya nyuklia.”
Trump pia alikanusha kuwa Marekani inatafuta kuongeza muda wa makubaliano ya muda yaliyofikiwa na Iran mwezi Juni.
Makubaliano hayo yalilenga kusitisha mara moja na kwa kudumu operesheni za kijeshi katika maeneo yote, lakini yalivunjika haraka. Trump alitangaza Julai 7 kuwa makubaliano hayo yamekwisha, wakati Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisema wiki moja baadaye kuwa yamesitishwa.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya awali, Marekani na Iran zilikubaliana kuendelea na mazungumzo ya kufikia makubaliano ya kudumu ndani ya siku 60, yakihusu pia masuala mapana zaidi, ikiwemo hatma ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Jumatatu ilikuwa siku ya 60 tangu kusainiwa kwa makubaliano hayo. Saa chache kabla, Trump aliambia mwandishi wa Fox News kupitia mahojiano ya simu kwamba Iran inapaswa “kuweka bendera nyeupe ya kujisalimisha.”
Wakati huo huo, Oman na Iran zimekuwa katika mazungumzo ya kutafuta makubaliano yatakayoruhusu kurejeshwa kwa usafirishaji wa kibiashara katika Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya kimataifa iliyokuwa ikipitisha takribani asilimia 20 ya mahitaji ya dunia ya mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa kabla ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kuanza mwishoni mwa Februari.
Trump alitoa onyo kali kwa Oman, akisema ikiwa nchi hiyo itaingilia suala hilo, Marekani ingechukua hatua za kijeshi dhidi yake.
Hata hivyo, alipoulizwa baadaye katika Ofisi ya Oval kama amepoteza uvumilivu kwa Oman, Trump alisema bado hana msimamo huo, ingawa alidai Oman haijafanya vizuri katika suala hilo.
Mzozo kuhusu udhibiti wa Mlango wa Hormuz umechangia kupanda kwa bei za mafuta na kuongeza shinikizo kwa Trump kutafuta njia ya kumaliza vita hivyo, ambavyo havipendwi na sehemu ya wananchi wa Marekani, kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Novemba.
Trump amesisitiza kuwa uchaguzi huo hauathiri mkakati wake kuhusu Iran.
“Uchaguzi wa katikati ya muhula hauhusiani kabisa na namna ninavyofikiri,” alisema.
Mapema Jumatatu, Trump pia aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social kwamba lengo namba moja la Marekani ni kuhakikisha Iran haiwezi, kwa namna yoyote, kumiliki silaha ya nyuklia—akirejea moja ya sababu kuu anazotumia kueleza msimamo wake dhidi ya Iran.