
Kinshasa, 17 Agosti 2026: Airtel Africa imeandika historia baada ya kuwa kampuni ya kwanza ya mawasiliano barani Afrika kuzindua kibiashara intaneti ya satelaiti kwa simu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ikifungua ukurasa mpya katika upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo yasiyofikiwa na minara ya kawaida ya simu.
Huduma hiyo, inayotolewa kupitia ushirikiano kati ya Airtel Africa na Starlink, inawezesha wateja wenye simu janja zinazooana kupata huduma za mawasiliano katika maeneo ambayo hayafikiwi na miundombinu ya kawaida ya mawasiliano ya simu.
Starlink ina zaidi ya satelaiti 650 zinazosaidia huduma za mawasiliano ya moja kwa moja kati ya satelaiti na simu (satellite-to-mobile). Kwa sasa, huduma hiyo inalenga matumizi ya programu zinazotumia kiwango kidogo cha data, ikiwemo ujumbe wa WhatsApp, pamoja na SMS, bila kuhitaji wateja kuwa na vifaa maalumu au kifaa cha ziada.
Uzinduzi huo unafuatia makubaliano ya kimkakati yaliyotangazwa na Airtel Africa na Starlink mwezi Desemba 2025, pamoja na majaribio ya huduma za data na ujumbe nchini Kenya mwezi Machi 2026.
DRC imekuwa soko la kwanza la Airtel Africa na nchi ya kwanza barani Afrika ambako huduma ya intaneti ya satelaiti kwa simu (Starlink Mobile) imefikia hatua ya kutolewa kibiashara.
Akizungumza kuhusu uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema hatua hiyo ni muhimu katika kupanua upatikanaji wa mawasiliano barani Afrika.
“Uzinduzi wa kwanza kabisa wa kibiashara wa Starlink Mobile barani Afrika ni hatua muhimu kwa Airtel Africa kupitia ushirikiano wetu na SpaceX. Kwa kuunganisha mtandao wa Airtel wa ardhini na teknolojia ya satelaiti ya Starlink, tunapanua upatikanaji wa mawasiliano muhimu zaidi ya mipaka ya miundombinu ya kawaida ya simu. DRC inaongoza katika hatua hii muhimu ya maendeleo, na uzoefu unaopatikana hapa utasaidia katika kupanua huduma hii hatua kwa hatua katika masoko yetu, kwa kuzingatia idhini za mamlaka za udhibiti za kila nchi.
“Ninapenda kutambua kwa namna ya pekee na kutoa shukrani zangu kwa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa msaada wake muhimu katika kufanikisha hatua hii, hususan kupitia Mheshimiwa Waziri wa Posta, Mawasiliano na Teknolojia Mpya ya Habari na Mawasiliano, Rais wa Mamlaka ya Udhibiti pamoja na timu zao.”
Taldar alisema uzoefu unaopatikana DRC utasaidia Airtel Africa katika kupanua huduma hiyo katika masoko mengine ya kampuni, kwa kuzingatia idhini na matakwa ya mamlaka za udhibiti katika kila nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel DRC, Thierry Diasnoma, alisema huduma hiyo ya satelaiti itaongeza fursa za mawasiliano katika nchi yenye eneo kubwa kijiografia, ambako baadhi ya wananchi wanaishi, kufanya kazi au kusafiri mbali na miundombinu ya kawaida ya mawasiliano.
“Huduma hii ya intaneti ya satelaiti kwa simu inatoa safu ya ziada ya mawasiliano, ikisaidia wateja kuendelea kupatikana, kupata taarifa na kuwasiliana katika maeneo ambayo mtandao wa minara haupatikani,” alisema Diasnoma.
Huduma ya intaneti ya satelaiti kwa simu inalenga pia kuwasaidia wasafirishaji na kampuni za usafirishaji na usambazaji, mashirika ya kibinadamu, wahudumu wa afya, wakulima, kampuni za uchimbaji madini na jamii zinazoishi katika maeneo ambayo hayajafikiwa kikamilifu na mitandao ya ardhini.
Aidha, teknolojia ya intaneti ya satelaiti kwa simu inaweza kuwa nyenzo muhimu katika mawasiliano ya dharura wakati wa majanga ya asili au pale ambapo mtandao wa kawaida unakatika kwa muda.
Kwa sasa, wateja wanaotaka kutumia huduma hiyo wanapaswa kuwa na simu janja ya Android yenye LTE inayooana na mfumo wa Starlink Mobile, pamoja na kifurushi cha data cha Airtel DRC kinachokidhi vigezo au huduma ya data roaming iliyowashwa.
Airtel imesema simu na vifaa vya kampuni ya Apple, vitawezeshwa kutumia huduma ya intaneti ya satelaiti kwa simu katika siku zijazo.
Wateja wanaokidhi vigezo wanaweza kujisajili kupitia MyAirtel App na kupata huduma ya majaribio bila malipo kwa siku 30 za kwanza.
Wateja wanaosafiri kwenda DRC na kujiunga na Airtel DRC wanaweza pia kujisajili kwa huduma hiyo ya majaribio baada ya kuamilisha huduma inayokidhi vigezo na kupakua MyAirtel App.
Baada ya kipindi cha majaribio, huduma itaendelea kupatikana kupitia vifurushi vya data vya Airtel vinavyokidhi masharti.
Airtel Africa na Starlink zimesema zinaendelea kuboresha huduma hiyo, huku uwezo wa ziada ukitarajiwa kuongezwa kadri teknolojia inavyoendelea kukua na idhini za udhibiti zinavyopatikana.
Uzinduzi huo unaiweka Airtel Africa katika nafasi ya kampuni ya kwanza ya mawasiliano barani Afrika kuanza kutoa intaneti ya satelaiti kwa simu kibiashara, huku ikiendelea kutumia teknolojia mpya kupanua wigo wa mawasiliano na kuongeza ujumuishwaji wa kidijitali barani Afrika.