
Kocha wa timu ya taifa ya Misri, Hossam Hassan, ameripotiwa kuanguka na kuzimia baada ya wake zake wawili kuingia katika ugomvi mkubwa uliogeuka kuwa mapambano ya kuvutana nywele mbele ya watalii waliokuwa hotelini.
Tukio hilo linadaiwa kutokea katika hoteli ya kifahari eneo la Porto Marina, kwenye pwani ya kaskazini mwa Misri, wakati Hassan akiwa likizo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, ugomvi ulianza kati ya mke wake wa muda mrefu, Howaida Al-Gharbawi, na mke wake wa pili, Dina “Dan Adam” Mustafa, kabla ya kuzichapa hotelini.

Ndugu waliingilia kati kujaribu kuwatenganisha, huku walinzi wa hoteli wakifika kudhibiti hali hiyo. Wanawake hao wawili waliripotiwa kupata majeraha madogo na michubuko.
Taarifa za awali zilidai kuwa Hassan alizimia alipokuwa akijaribu kuzuia ugomvi huo, huku tukio hilo likielezwa kuwa limemsababishia msongo mkubwa wa mawazo.
Hata hivyo, wakili wa Hassan alikanusha taarifa kwamba kocha huyo alikuwa amepata tatizo kubwa la kiafya, akisema yuko katika hali nzuri.

Baada ya tukio hilo, Hassan ameripotiwa kuachana na mke wake wa kwanza, Howaida, na inadaiwa alisaini rasmi nyaraka za talaka katika ofisi ya msajili wa ndoa mjini Cairo.
Hassan na Howaida walikuwa pamoja kwa miongo kadhaa na wana watoto watatu.
Wakati huo huo, Mohamed Shams, wakili wa mke wa pili, Dan Adam, amesema walikuwa wameamini suala hilo lisingefikia hatua ya talaka, lakini mambo yalizidi kuwa mabaya.
Hassan alimuoa Dan Adam mwaka 2015, wakati bado alikuwa kwenye ndoa na Howaida. Wawili hao waliwahi kutengana mwaka 2022 kabla ya kurudiana.

Kwa mujibu wa sheria ya Misri, mwanaume Mwislamu anaruhusiwa kisheria kuwa na wake hadi wanne kwa wakati mmoja, huku akiwa na wajibu wa kuwahudumia kwa usawa katika masuala kama makazi, matumizi na viwango vya maisha.
Hossam Hassan amekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Misri tangu mwaka 2024. Anaendelea kuiongoza timu hiyo na inadaiwa amesaini mkataba mpya utakaomuweka kwenye nafasi hiyo hadi mwaka 2030.