×

UAE Yasimamisha Shughuli Zote za Biashara na Iran, Waziri Afunguka

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Beqai

Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umetangaza kusitisha shughuli zote za kibiashara na kifedha na Iran hadi itakapotangaza vinginevyo, huku mivutano ya kijeshi katika Mashariki ya Kati ikiendelea kuongezeka.

Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE imesema uamuzi huo umetokana na kuongezeka kwa mivutano katika eneo hilo, ambayo imeelezwa kuwa inahatarisha amani na usalama wa kikanda.

Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya Wizara ya Ulinzi ya UAE kusema kuwa Iran ilirusha makombora mawili ya masafa marefu kuelekea UAE.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kombora moja liliangukia nje ya maji yaliyo chini ya mamlaka ya UAE, huku jingine likiangukia ndani ya maji ya nchi hiyo.

Hata hivyo, Iran imekanusha madai hayo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Beqai, amesema madai ya UAE hayana msingi.

“Madai ya Umoja wa Falme za Kiarabu hayana msingi,” Beqai alisema katika taarifa.

Uamuzi wa UAE unakuja wakati mzozo kati ya Iran, Marekani na Israel ukiendelea kuathiri usalama wa Mashariki ya Kati, huku nchi za Ghuba zikijikuta katika mazingira magumu kutokana na ukaribu wao wa kijiografia na Iran.

UAE imekuwa miongoni mwa nchi za eneo hilo zilizokumbwa na athari za mzozo huo, huku mashambulizi na vitisho vya kijeshi vikiongeza hofu kuhusu usalama wa nchi na shughuli za biashara katika eneo hilo.

Hata hivyo, Iran haikuishambulia UAE katika operesheni hiyo baada ya kusainiwa kwa mkataba wa maelewano, hatua iliyosaidia kupunguza hatari ya mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya nchi hiyo.

Leave a Comment