
Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, amekataa hoja kwamba Rais wa Tanzania hawezi kupelekewa wito wa mahakama, akisema Rais anaweza kupelekewa wito huo kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Lissu amesema kwa upande wa Rais, wito unaweza kupelekwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi au Katibu Binafsi wa Rais, ambaye anaweza kusaidia mahakama kumfikishia Rais wito huo.
Amesema ni kweli kwamba wito wa mahakama hauwezi kumpelekea Rais moja kwa moja, bali unaweza kuwasilishwa kupitia katibu wake.
Lissu amekiri kwamba mahakama haiwezi kumlazimisha Rais kufika mahakamani, lakini inaweza kumpelekea wito kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
“Na Rais ndiye ataamua kuuheshimu wito huo au la,” amesema Lissu.
Kuhusu Makamu wa Rais mstaafu na Waziri Mkuu mstaafu, Lissu amesema tayari wamestaafu na hivyo hawawezi kutumia hoja kwamba wanamsaidia Rais katika utekelezaji wa majukumu yake.
Vilevile, Lissu ametoa hoja kuhusu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkurugenzi wa Ujasusi, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkuu wa Majeshi, akisema wote wanaweza kuitwa mahakamani kama mashahidi.
Lissu amesema hakuna mtu au afisa yeyote ambaye hawezi kupelekewa wito wa mahakama, akiwamo Rais, Makamu wa Rais mstaafu, Mkuu wa Majeshi au Mkuu wa Jeshi la Polisi.
Amesema mahakama inaweza kutoa wito kwa Rais, ingawa haina uwezo wa kutoa hati ya kukamatwa dhidi yake.
Hata hivyo, kwa mujibu wa hoja zake, Makamu wa Rais mstaafu, Waziri Mkuu mstaafu, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Majeshi na Mkuu wa Ujasusi wanaweza kupewa hata hati ya kukamatwa iwapo mazingira ya kisheria yatatimia.
Lissu ameiambia mahakama kwamba ikiwa haiwezi kutoa wito kwa mashahidi aliowaomba kutoka upande wa Serikali ili wafike mahakamani, basi haki katika kesi hiyo inaweza kuathirika.
“Kama kwenye kesi kubwa kama hii mahakama haiwezi kupeleka wito, basi sijui itaonekanaje. Lindeni haki yangu ili kuweka haki katika kesi na uadilifu,” amesema Lissu.
Ameeleza kuwa hakuna shauri linalozuia mashahidi kupelekewa wito wa mahakama, akisisitiza kuwa mashahidi hao wanaweza kuitwa na kwamba ushahidi wao ni muhimu katika kesi hiyo.