×

Rais Samia Azindua Bwawa la Julius Nyerere, Atoa Tahadhari ya El Niño (Picha +Video)


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi, wageni mbalimbali pamoja na wananchi waliohudhuria hafla ya Uzinduzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2115 katika eneo la Rufiji mkoani Pwani tarehe 22 Agosti, 2026.

PWANI: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kukamilika kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) ni utekelezaji wa ndoto ya muda mrefu ya Tanzania ya kuwa na nishati ya uhakika kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Rais Samia amesema hayo leo, Jumamosi, Agosti 22, 2026, wakati akizindua rasmi mradi huo uliopo mkoani Pwani.

Amesema Serikali ilipa mradi huo uzito unaostahili kutokana na umuhimu wake kwa Taifa, akisisitiza kuwa haukuwa mradi wa kuachwa kwa sababu una mchango mkubwa katika kuongeza umeme kwenye Gridi ya Taifa.

Rais  Samia  akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP).

Rais Samia amekumbusha kuwa Desemba 22, 2022 alifika eneo la mradi kushuhudia hatua ya kufungwa kwa njia ya kuchepusha maji ya Mto Rufiji na kuanza kujazwa kwa bwawa.

Alisema awali ilitarajiwa bwawa hilo kujazwa ndani ya miaka mitatu, lakini kwa neema ya Mungu lilijaa ndani ya mwaka mmoja na nusu, jambo lililowezesha majaribio ya uzalishaji umeme kuanza mapema.

Katika hafla hiyo, Rais Samia alizindua rasmi kituo cha kuzalisha umeme na kukagua maeneo mbalimbali ya mradi, yakiwemo mitambo ya uzalishaji, tuta kuu pamoja na kituo cha kupokea na kusafirisha umeme kwenda kwenye Gridi ya Taifa.

Amesema maeneo hayo yanafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kwamba mradi huo ni jambo la kujivunia kwa Taifa.

JNHPP ina uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, hali inayoongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Tanzania katika kuhudumia mahitaji ya nishati kwa shughuli za uzalishaji, viwanda, uwekezaji na maendeleo ya wananchi.

Samia awakumbuka viongozi waliotangulia

Rais Samia amesema kukamilika kwa mradi huo kunatoa somo kuhusu umuhimu wa kuwa na nidhamu katika ufuatiliaji wa miradi, ustahimilivu katika kukabiliana na changamoto na uimara wa kusimamia malengo ya miradi ya kimkakati.

Amesema kuanzisha mradi pekee hakutoshi, bali matokeo yake hutegemea namna Serikali inavyofuatilia utekelezaji wake hatua kwa hatua hadi kufikia malengo yaliyowekwa.

Rais Samia pia amewashukuru viongozi wa awamu zilizopita kwa kuendeleza maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ya kutumia rasilimali za Mto Rufiji kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Miongoni mwa viongozi aliowataja ni Hayati Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin Mkapa na Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, kwa mchango wao katika kuendeleza dira hiyo.

Aidha, amemkumbuka na kumshukuru Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa msimamo wake wa kuhakikisha fedha zinapatikana na ujenzi wa mradi unaanza licha ya changamoto na upinzani uliokuwepo.

Samia atoa tahadhari kuhusu mvua kubwa

Katika hatua nyingine, Rais Samia amewataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Taasisi za Serikali kujiandaa mapema kukabiliana na uwezekano wa mvua kubwa zinazotabiriwa kunyesha nchini.

Amesema taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zinaonyesha uwezekano wa mvua kubwa zinazohusishwa na mfumo wa hali ya hewa wa El Niño.

Rais Samia amesisitiza kuwa taarifa hizo zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito na hatua za tahadhari zichukuliwe kabla ya madhara kujitokeza.

Ameagiza viongozi kuhakikisha mifereji inasafishwa, mifumo ya uokoaji inaandaliwa na wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi wanatambuliwa na kuondolewa mapema.

“Niwaombe nendeni mkajitayarishe, mkaweke mazingira sawa ili mvua hizo zitakapoanza zisilete maafa makubwa kwa wananchi wetu,” amesema Rais Samia.

Amesisitiza kuwa tahadhari zinazotolewa na TMA zinapaswa kufanyiwa kazi kwa wakati ili kulinda maisha na mali za wananchi.

Maelekezo hayo yametolewa muda mfupi baada ya Rais Samia kukamilisha uzinduzi rasmi wa JNHPP, mradi unaotarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa umeme na kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini.

Leave a Comment