×

Kadi Nyekundu Zatikisa Simba Wachezaji Watatu Nje, Waibua Maswali

Simba SC imeanza msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kasi kubwa baada ya kushinda michezo yake yote mitatu ya mwanzo. Hata hivyo, mwenendo wa kupata kadi nyekundu katika kila mchezo umeanza kuibua maswali kuhusu nidhamu ya kikosi hicho.

Katika michezo yake mitatu ya mwanzo ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2026/27, Simba SC imekumbana na kadi nyekundu katika kila mchezo, lakini jambo la kuvutia ni kwamba imeshinda yote na kufikisha alama tisa.

Mchezo wa kwanza: Kagera Sugar 0-2 Simba SC

Simba ilianza kampeni zake kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Agosti 16, 2026. Ismail Touré alifunga bao la kwanza dakika ya 45, kabla ya Elie Mpanzu kuongeza la pili dakika ya 69.

Hata hivyo, dakika ya 55, beki David Kameta ‘Duchu’ alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumchezea madhambi David Luhende. Licha ya kucheza pungufu, Simba ilifanikiwa kulinda ushindi wake.

Mchezo wa pili: Pamba Jiji 1-2 Simba SC

Katika mchezo wa pili uliochezwa Agosti 19, Simba ilishinda 2-1 dhidi ya Pamba Jiji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Clatous Chama aliipa Simba bao la kwanza dakika ya 18, kabla ya Anicet Oura kuongeza la pili dakika ya 30. Pamba Jiji ilipata bao la kufutia machozi kupitia Idriss Diomande kwa mkwaju wa penalti.

Dakika ya 44, Simba ilibaki na wachezaji 10 baada ya Ibraheem Jabaar kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kufuatia tukio la kumgonga mpinzani kwa kiwiko. Pamoja na kucheza pungufu, Simba ilishikilia ushindi wa 2-1.

Mchezo wa tatu: Singida Black Stars 1-2 Simba SC

Katika mchezo wa tatu, Simba iliendeleza ushindi wake baada ya kuifunga Singida Black Stars 2-1 katika mchezo uliochezwa Agosti 22, 2026.

Clatous Chama aliifungia Simba bao la kwanza dakika ya 12, lakini Singida ikasawazisha kupitia Sheikhan dakika ya 22. Simba ilipata bao la ushindi dakika ya 62 kupitia Rushine De Reuck kwa mkwaju wa penalti.

Dakika ya 85, beki wa Simba Anthony Mligo alionyeshwa kadi nyekundu kufuatia rafu mbaya, na hivyo Simba kumaliza mchezo ikiwa na wachezaji 10. Pamoja na hilo, ilifanikiwa kushikilia ushindi wa 2-1 na kufikisha alama tisa katika michezo mitatu.

Kwa hiyo, katika michezo hiyo mitatu, Simba imefunga mabao sita na kufungwa mabao mawili, huku wachezaji wake watatu David Kameta, Ibraheem Jabaar na Anthony Mligo wakipewa kadi nyekundu.

Mfululizo huo unaifanya Simba kuwa na mwanzo mzuri kwa upande wa matokeo, lakini pia unaweka alama ya kuuliza kuhusu nidhamu ya wachezaji, kwani katika kila mchezo timu imelazimika kucheza sehemu ya muda ikiwa na pungufu ya mchezaji.

Stori na Ashura Karimu| GPL – TUDACO

Leave a Comment