×

Jamal Bakhresa Afungiwa Kujihusisha na Mpira kwa Mwaka Mmoja

Kiongozi wa Azam FC, Jamal Bakhresa, amefungiwa kujihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Agosti 22, 2026, adhabu hiyo inahusishwa na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyodaiwa kufanywa na Bakhresa kabla na baada ya mchezo wa fainali ya Kombe la CRDB uliochezwa kisiwani Pemba.

Bakhresa alifikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu ya TFF kujibu tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa kanuni za nidhamu. Katika mchakato wa kusikilizwa kwa shauri hilo, alisaidiwa na Wakili Alex Mushumbusi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bakhresa alikiri baadhi ya makosa yaliyowasilishwa mbele ya kamati hiyo.

Mbali na adhabu ya kufungiwa kujihusisha na shughuli za mpira kwa mwaka mmoja, Bakhresa pia ameamriwa kulipa faini kutokana na makosa yaliyobainishwa. Aidha, ameahidi kutorudia vitendo hivyo.

Kamati ya Nidhamu ya TFF imesema uamuzi huo umetolewa kwa kuzingatia Ibara ya 11(f) ya Kanuni za Nidhamu za TFF, Toleo la mwaka 2021.

Adhabu hiyo inamaanisha Bakhresa hataruhusiwa kushiriki katika shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi kilichowekwa na kamati, huku uamuzi huo ukilenga kuimarisha nidhamu na kuzingatiwa kwa kanuni katika soka la Tanzania.

Stori na Florah Anderson | GPL – TUDACO

Leave a Comment