Mwanamuziki wa Bongo Flava, Juma Jux, na mke wake Priscilla Ojo, maarufu kama Priscy, wamezua gumzo mitandaoni baada ya kuamua kuonyesha sura ya mtoto wao kwa mara ya kwanza tangu kuzaliwa.
Kwa miezi kadhaa, wawili hao walikuwa wamechagua kutoweka wazi sura ya mtoto wao, jambo lililowaacha mashabiki na wafuasi wao wakisubiri kwa hamu kumuona.

Hata hivyo, Jux na Priscy sasa wamevunja ukimya huo baada ya kushirikisha picha rasmi ya mtoto wao iliyopigwa kwa mtindo wa kitaalamu na kuvutia hisia za watu wengi kwenye mitandao ya kijamii.
Uamuzi huo umeongeza gumzo miongoni mwa mashabiki, huku wengi wakieleza furaha yao baada ya hatimaye kupata nafasi ya kumuona mtoto huyo ambaye amekuwa akifichwa kwa muda.

Mbali na sura yake, mavazi na muonekano wa mtoto huyo pia yamezua mjadala, huku baadhi ya mashabiki wakigusia maisha ya kifahari yanayoonekana katika familia ya Jux na Priscy.
Priscy, ambaye anatokea nchini Nigeria, amejijengea jina katika mitindo, biashara na ushawishi kupitia mitandao ya kijamii. Yeye ni binti wa mwigizaji maarufu wa Nollywood, Iyabo Ojo.
Licha ya kukulia katika familia yenye umaarufu, Priscy amefanikiwa kujenga chapa yake binafsi katika ulimwengu wa mitindo na burudani, huku uhusiano wake na Jux ukiendelea kuvuta hisia za mashabiki Tanzania na Nigeria.
