×

Netanyahu Aingia Mtegoni, Uturuki Yataka Interpol Imkamate

Uturuki imetangaza hatua ya kutaka Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akamatwe kimataifa kufuatia uchunguzi kuhusu shambulio dhidi ya wanaharakati waliokuwa wakipeleka misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Waziri wa Sheria wa Uturuki, Akin Gurlek, amesema hati za kukamatwa zimetolewa dhidi ya Netanyahu pamoja na mshukiwa mwingine, kwa tuhuma zinazohusisha mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mateso.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kesi hiyo inawahusisha jumla ya watu 35 na inahusiana na tukio la Israel kuingilia boti za Global Sea Flotilla katika maji ya kimataifa wakati zikiwa njiani kuelekea Gaza kwa ajili ya kupeleka misaada ya kibinadamu.

Uturuki imekuwa mkosoaji mkubwa wa operesheni za kijeshi za Israel nchini Gaza, huku serikali yake ikiendelea kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya kile inachodai kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Hatua hiyo ya Uturuki inatarajiwa kuongeza mvutano wa kisheria na kidiplomasia kati ya nchi hiyo na Israel, huku suala la kukamatwa kwa Netanyahu likiwa sasa likielekezwa kwenye taratibu za kimataifa kupitia Interpol.

Hata hivyo, Israel imeendelea kukataa tuhuma za kufanya ukiukaji wa sheria za kimataifa na haki za binadamu, jambo linalofanya hatua hiyo ya Uturuki kuwa suala linaloweza kuendelea kujadiliwa katika ngazi za kimataifa.

Stori na Ilankize Godfrey | GPL – TUDACO

Leave a Comment