×

Rais wa UEFA Čeferin Amtaka Infantino Kujiuzulu Urais wa FIFA

Rais wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), Aleksander Čeferin, amemtaka Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kujiuzulu nafasi hiyo, huku akisema hana mpango wa kugombea urais wa FIFA dhidi yake.

Čeferin ametoa kauli hiyo wakati Infantino akikabiliwa na shinikizo la kuondoka madarakani kufuatia mpango uliositishwa wa kuuza hisa katika Kombe la Dunia kwa wawekezaji binafsi.

Mashirikisho matatu ya soka ya mabara yameupinga mpango huo, yakidai kulikuwa na udanganyifu, huku UEFA ikitishia kususia baadhi ya mashindano yanayoandaliwa na FIFA.

Akizungumza katika mahojiano na podcast nchini Uingereza, Čeferin amesema Infantino amepoteza uungwaji mkono wa baadhi ya wadau muhimu wa soka, wakiwemo mashabiki, wachezaji na makocha.

Hata hivyo, Čeferin amesema hana nia ya kuwania urais wa FIFA, akieleza kuwa anaipenda nafasi yake ndani ya UEFA na pia anataka kupata muda wa kufurahia maisha nje ya majukumu ya uongozi wa soka.

Infantino amekuwa Rais wa FIFA tangu mwaka 2016. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwisho wa kuwasilisha fomu za wagombea katika uchaguzi huo ni Novemba 18.

Čeferin, mwenye umri wa miaka 58, amesisitiza kuwa licha ya kutokuwa tayari kugombea nafasi hiyo, anaamini wakati umefika kwa Infantino kuachia madaraka ya uongozi wa soka duniani.

Stori na Ilankize Godfrey | GPL – TUDACO

Leave a Comment