Mtoto wa mastaa Kim Kardashian na Kanye West, North West, amesema anatamani kuwa na maisha ya kawaida na kupata kazi ya kawaida, licha ya kuwa tayari ameanza kujijengea jina katika ulimwengu wa burudani akiwa na umri mdogo.
North, ambaye kwa sasa ana miaka 13, amefichua kuwa anatamani kufanya kazi katika katika kampuni ya kuuza kahawa mwaka ujao, akisema anataka kupata uzoefu wa kuwa na “kazi ya kawaida” kama watu wengine.

Akizungumza katika mahojiano yake na jarida la Dazed, North alisema bado ana hamu ya kufanya kazi na kwamba moja ya ndoto zake ni kuwa mhudumu wa kahawa.
“Bado nataka kufanya kazi. Nataka kufanya kazi Starbucks mwaka ujao. Nafikiri naweza kwa sababu nitakuwa na miaka 14. Nataka kuwa na kazi ya kawaida, nadhani,” alisema North.
Kauli hiyo imekuja licha ya North tayari kuanza safari yake katika ulimwengu wa umaarufu. Amejishughulisha na muziki, amewahi kushiriki katika maonesho ya jukwaani na pia kuonekana katika maudhui mbalimbali ya mitindo.
Kutokana na wazazi wake kuwa miongoni mwa watu maarufu duniani, North amekuwa akifuatiliwa na vyombo vya habari tangu akiwa mtoto.
Hata hivyo, sasa anaonekana kutamani kupata uzoefu tofauti na maisha ya umaarufu, akitaka kujua namna watu wengine wanavyoishi na kufanya kazi za kawaida.
Katika mahojiano hayo, North pia alizungumzia mwonekano wake, ikiwemo nywele zake za bluu na ambazo zimekuwa zikizungumziwa mitandaoni.
Akijibu wanaokosoa mwonekano huo, alisema watu wengi wanafanya mambo mengine anayoyaona kuwa mabaya, huku yeye akisisitiza kuwa anachotaka ni kuwa na nywele za bluu.
Licha ya kuwa bado ni kijana, North tayari ameanza kujenga utambulisho wake nje ya umaarufu wa wazazi wake, huku kauli yake kuhusu kutaka kufanya kazi Starbucks ikionyesha namna anavyotamani kupata maisha yenye uzoefu wa kawaida.