
Watoto wachanga 14 wamefariki dunia baada ya moto mkubwa kulipuka katika wodi ya kujifungulia na kuhudumia watoto wachanga katika Hospitali ya Pakistan Institute of Medical Sciences (PIMS), jijini Islamabad, Pakistan.
Moto huo umetokea leo Jumatano, Agosti 26, 2026, majira ya saa 6:45 asubuhi, ambapo taarifa za awali zinaeleza kuwa ulianzia kwenye mfumo wa kiyoyozi katika kitengo cha kujifungua.
Wakati moto ukianza, jumla ya watoto wachanga 15 walikuwa katika wodi hiyo. Kwa mujibu wa msemaji wa hospitali, watoto 14 walishindwa kuokolewa huku mmoja akiokolewa na daktari.

Waokoaji walifika hospitalini hapo kwa kutumia magari sita ya zimamoto na magari ya wagonjwa manne. Watu wengine 19, wakiwemo wanawake 10, watoto saba na wanaume wawili, waliokolewa na kupelekwa sehemu salama.
Polisi wameeleza kuwa miili ya watoto waliofariki imeungua vibaya, hivyo vipimo vya DNA vitatumika katika utambuzi kabla ya miili hiyo kukabidhiwa kwa wazazi.
Tukio hilo limezua maswali kuhusu usalama wa moto katika hospitali hiyo. Baadhi ya wazazi wamedai kuwa milango ya wodi hiyo ilikuwa imefungwa na kwamba hakukuwa na maandalizi ya kutosha ya kukabiliana na moto.

Hata hivyo, uongozi wa hospitali umekanusha madai hayo, ukisema mlango haukuwa umefungwa bali ulikuwa ukilindwa na mhudumu kwa lengo la kuhakikisha watoto wachanga hawaibiwi.
Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ametoa pole kwa familia za waathirika na kuagiza uchunguzi wa haraka ili kubaini kilichosababisha janga hilo.
Rais wa Pakistan, Asif Ali Zardari, pia ameeleza masikitiko yake na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usalama dhidi ya moto katika hospitali, hususan katika maeneo yanayohudumia watoto wachanga.

Kamati maalumu imeundwa kuchunguza tukio hilo na inatarajiwa kuwasilisha ripoti ndani ya saa 24, ikiwemo kubaini chanzo cha moto na kama vifaa vya usalama dhidi ya moto vilikuwepo na vilikuwa vinafanya kazi ipasavyo.
Stori na Florah Anderson | GPL -TUDACO