×

Harmonize Afichua Wasanii Walio kwenye Albamu Yake Mpya “31”

Msanii wa Bongo Fleva, Harmonize, ameweka wazi orodha ya nyimbo zitakazopatikana katika albamu yake mpya inayokwenda kwa jina la “31”, ambayo inatarajiwa kutoka hivi karibuni.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize ameshirikisha mashabiki wake orodha ya nyimbo 14 zitakazounda albamu hiyo, huku akitangaza kuwa inatarajiwa rasmi kutoka Septemba 4, 2026.

Albamu hiyo imebeba ushirikiano mbalimbali kutoka kwa wasanii wakubwa ndani na nje ya Tanzania, akiwemo Marioo, Young Lunya, Jay Melody, Mayorkun, Darkoo, Yemi Alade, Rayvanny na Sofia Nzau, pamoja na wasanii wengine.

Kwa mujibu wa orodha hiyo, Harmonize anatarajiwa kuendelea kuonyesha uwezo wake wa kuunganisha muziki wa Bongo Fleva na ladha mbalimbali za kimataifa kupitia nyimbo zitakazopatikana kwenye albamu hiyo.

Harmonize, ambaye ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa kujenga jina kubwa katika muziki wa Tanzania, tayari ameachia albamu kadhaa zilizofanya vizuri, zikiwemo “Afro East” iliyotoka mwaka 2020, “High School” mwaka 2021 na “Made For Us” mwaka 2022.

Kwa sasa, Harmonize anaendelea kufanya vizuri kupitia wimbo wake “Beautiful”, ambao pia umejumuishwa katika albamu mpya ya “31”.

Albamu hiyo inatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya Harmonize kwa mwaka huu, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona namna atakavyowasilisha kazi hizo mpya pamoja na ushirikiano wa wasanii mbalimbali.

Stori na Na Didas Didas | GPL

Leave a Comment