×

Mkuu wa CIA Afanya Ziara ya Siri Moscow, Putin Apewa Onyo Kali

Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), John Ratcliffe, ameripotiwa kufanya ziara ya siri mjini Moscow kwa kutumia ndege ya kijeshi ya Marekani, huku akikutana na viongozi wakuu wa ujasusi wa Urusi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na The Wall Street Journal na The New York Times, Ratcliffe alipeleka ujumbe mzito kwa Moscow kuhusu vita vya Ukraine na mahusiano ya Urusi na NATO.

Inadaiwa kuwa katika mazungumzo hayo, Ratcliffe aliionya Urusi kutoshambulia nchi wanachama wa NATO, huku taarifa nyingine zikisema aliiambia Moscow kutathmini upya msimamo wake katika vita vya Ukraine na kutafuta makubaliano kabla hali yake ya kijeshi na kiuchumi haijawa mbaya zaidi.

Ratcliffe aliripotiwa kukutana na Aleksandr Bortnikov, mkuu wa shirika la usalama la ndani la Urusi, FSB. Rais wa Urusi, Vladimir Putin, hakukutana moja kwa moja na Ratcliffe, lakini alielezwa kuhusu mazungumzo hayo.

Ziara hiyo ilifanyika baada ya ndege ya kijeshi ya Marekani aina ya C-17 Globemaster III kutua katika Uwanja wa Ndege wa Vnukovo, Moscow, ikitokea Riga nchini Latvia.

Baada ya ndege hiyo kutua, msafara wa magari yenye namba za kidiplomasia za Marekani ulionekana ukielekea katikati ya Moscow, jambo lililoibua taharuki na maswali kuhusu sababu ya ziara hiyo ya ghafla.

Rais Donald Trump baadaye aliielezea safari hiyo kama ziara ya “semi-routine”, lakini akaashiria kuwa huenda kukawa na matokeo muhimu kutokana na mazungumzo hayo.

Ziara ya Ratcliffe inakuja wakati jitihada za kidiplomasia za kumaliza vita vya Ukraine zikiwa bado zinaendelea, huku Marekani ikijaribu kuishawishi Moscow na Kyiv kuelekea makubaliano ya kusitisha mapigano.

Safari hiyo pia inakumbusha ziara ya aliyekuwa Mkurugenzi wa CIA, William Burns, mjini Moscow mwaka 2021, ambapo aliripotiwa kumuonya Putin kuhusu madhara ya kuivamia Ukraine.

Leave a Comment