×

Wanafunzi Ihowanja Wapata Madarasa, Madawati Kutoka Vodacom

Mkuu wa Kanda ya Kati wa Vodacom Tanzania PLC, Chiha Nchimbi (kulia), akikabidhi dawati kwa Diwani wa Kata ya Kilosampepo, Boniventure Killian Mwanga (kushoto), dawati hilo ni mojawapo ya madawati 30 yaliyokabidhiwa katika Shule ya Msingi Ihowanja, Malinyi mkoani Morogoro, kupitia mpango wa Classroom for impact ulioko chini ya Vodacom Tanzania Foundation.

Vodacom Tanzania PLC, kupitia programu ya Classroom for Community Impact iliyo chini ya Vodacom Tanzania Foundation, imekabidhi madarasa mawili yaliyokarabatiwa, madawati 30 pamoja na vifaa muhimu vya shule kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Ihowanja, wilayani Malinyi, mkoani Morogoro.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kampuni hiyo katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi za umma nchini, hususan kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Makabidhiano hayo yaliyofanyika jana yanalenga kuchangia uboreshaji wa miundombinu na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi, ili kuwawezesha kupata elimu katika mazingira salama na rafiki.

Kupitia mpango huo, katika awamu hii Vodacom Tanzania imekarabati na kujenga jumla ya madarasa sita pamoja na kutoa madawati 90 katika shule tatu za msingi za umma za Vikindu, wilayani Mkuranga mkoani Pwani; Ihowanja, wilayani Malinyi mkoani Morogoro; na Mahilo, wilayani Songea mkoani Ruvuma.

Katika Shule ya Msingi Ihowanja, msaada huo umehusisha ukarabati wa madarasa mawili na utoaji wa madawati 30. Aidha, wanafunzi wamepatiwa mahitaji muhimu ya shule, ikiwemo madaftari, chupa za kubebea maji, kalamu na mabegi.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Kanda ya Kati wa Vodacom Tanzania PLC, Chiha Nchimbi, alisema mpango huo ni sehemu ya mchango wa kampuni katika kusaidia jamii na kuboresha mazingira ambayo watoto wanapata elimu.

Alisema uwepo wa madarasa salama, madawati ya kutosha na mazingira rafiki ya kujifunzia ni muhimu katika kuwawezesha wanafunzi, hasa wenye mahitaji maalum, kushiriki kikamilifu katika masomo yao.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ihowanja, Iddy Mgonja, aliishukuru Vodacom Tanzania kwa msaada huo, akisema utakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia shuleni hapo.

Mgonja alisema ukarabati wa madarasa mawili pamoja na kupatiwa madawati 30 na vifaa muhimu vya shule kutawawezesha wanafunzi kupata mazingira salama na rafiki zaidi ya kujifunzia, huku walimu wakipata mazingira bora ya kutekeleza majukumu yao ya kufundisha.

Kwa upande wa serikali na uongozi wa jamii, makabidhiano hayo yalishuhudiwa na Diwani wa Kata ya Kilosampepo, Boniventure Killian Mwanga, pamoja na Mtendaji wa Kijiji cha Ihowanja, Gotard Garus Mitti, viongozi na wadau wengine wa elimu.

Viongozi hao wamepongeza uwekezaji huo, wakisema utasaidia kupunguza changamoto za miundombinu ya elimu na kuweka mazingira bora na salama zaidi kwa wanafunzi na walimu.

Wamesisitiza kuwa ushirikiano kati ya sekta binafsi, serikali na jamii ni muhimu katika kuharakisha upatikanaji wa miundombinu bora na jumuishi ya elimu, hususan kwa watoto wenye mahitaji maalum.

Mpango wa Classroom for Community Impact ni sehemu ya jitihada za Vodacom Tanzania kupitia Vodacom Foundation za kushirikiana na jamii katika kuboresha mazingira ya elimu na kusaidia kujenga mazingira jumuishi zaidi ya kufundishia na kujifunzia kwa watoto nchini.

Leave a Comment