
Iringa, Agosti 25, 2026 — Umoja wa Madereva wa Malori nchini umemtunuku S/SGT Mongo cheti cha pongezi, tuzo pamoja na fedha taslimu Shilingi milioni moja, kwa kutambua mchango wake katika kurahisisha mtiririko wa magari na kuimarisha usalama barabarani.
Tuzo hiyo imetolewa kama ishara ya kuthamini utendaji wake katika kutekeleza majukumu ya usimamizi wa usalama barabarani, hususan katika maeneo yenye msongamano wa magari ya mizigo.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi, amempongeza S/SGT Mongo kwa utendaji wake na kuwataka madereva kuendelea kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.
Kamanda Bukumbi amesisitiza kuwa usalama barabarani ni jukumu la kila mtumiaji wa barabara, hivyo madereva wanapaswa kuwa waangalifu, kuheshimu sheria na kuhakikisha magari yao yanakuwa katika hali salama wakati wote.
Kwa upande wake, S/SGT Mongo amewashukuru madereva hao kwa kutambua juhudi zake na kusema kuwa tuzo hiyo imempa hamasa zaidi ya kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na kujituma.
Aidha, amemshukuru Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camillus Wambura kwa uongozi wake na mchango katika kuwawezesha askari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
S/SGT Mongo amesema utambuzi huo ni motisha kwake na kwa askari wengine kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kuhakikisha usalama wa watumiaji wote wa barabara.
Tukio hilo linaendelea kuonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wadau wa usafirishaji katika kuboresha usalama barabarani na kuhakikisha mtiririko mzuri wa magari katika barabara za Tanzania.