
DAR ES SALAAM — Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, leo Agosti 31, 2026, anaendelea kutoa ushahidi wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.
Mnyika alianza kutoa ushahidi wa utetezi Agosti 28, 2026, akiwa shahidi wa pili katika kesi hiyo, baada ya Lissu ambaye ni mshtakiwa katika kesi hiyo kumaliza kutoa sehemu yake ya utetezi.
Katika ushahidi wake, Mnyika ameliambia Mahakama kwamba yeye ndiye aliyeandaa Mkutano wa CHADEMA uliofanyika Aprili 3, 2025, ambao upande wa mashtaka umehusisha na kauli zinazodaiwa kuwa za uchochezi zilizotolewa na Lissu.
Mnyika amesema maandalizi ya mkutano huo yalikuwa chini yake, akieleza kuwa Lissu hakuwa mtu aliyehusika na maandalizi ya mkutano huo kama ambavyo imeelezwa katika baadhi ya hoja zinazowasilishwa katika kesi hiyo.
Iwapo Mnyika atamaliza kutoa ushahidi wake wa utetezi leo, hatua inayofuata itakuwa ni kuulizwa maswali ya dodoso na upande wa Jamhuri, ambao ndio unaendesha mashtaka dhidi ya Lissu.
Lissu anakabiliwa na mashtaka ya uhaini chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania, kama ilivyorekebishwa mwaka 2023.
Kesi hiyo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu kutokana na nafasi ya Lissu katika CHADEMA na uzito wa mashtaka yanayomkabili.