×

Kiongozi Wa Upinzani Akabiliwa Na Mashtaka Ya Uhaini Zambia

LUSAKA, Zambia — Mawakili wa kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile, wamethibitisha kuwa mteja wao amefikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la uhaini, wakati mvutano wa kisiasa ukiendelea kushika kasi nchini humo.

Wakili wake, Milner Katolo, amesema Mundubile yuko tayari kujitetea dhidi ya mashtaka hayo, huku akithibitisha taarifa hizo Jumamosi jioni katika mahojiano na Zambian Eye.

Mundubile alikamatwa Alhamisi kufuatia operesheni iliyofanywa na mamlaka, baada ya awali kujificha kufuatia hatua zilizokuwa zimechukuliwa dhidi yake.

Kiongozi huyo wa upinzani alikuwa miongoni mwa waliopinga matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni wa urais nchini Zambia, ambapo Rais Hakainde Hichilema alitangazwa mshindi na kupata muhula wa pili madarakani.

Mzozo huo wa kisiasa umeendelea kuongeza presha nchini Zambia, huku mamlaka zikikituhumu chama cha Mundubile, NRPUP, kwa kupanga uasi wa kutumia silaha.

Hata hivyo, chama hicho kimekanusha madai hayo na kupinga tuhuma zinazotolewa dhidi yake.

Kesi ya Mundubile sasa inatarajiwa kufuatiliwa kwa karibu, huku hatua za mahakama zikitoa mwelekeo wa namna mvutano huo wa kisiasa utakavyoendelea.

Leave a Comment