
Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20, Tanzanite Queens, imeondoka nchini kuelekea Poland tayari kwa fainali za Kombe la Dunia la FIFA U-20, zinazotarajiwa kuanza Septemba 5, 2026.
Tanzanite Queens imepangwa katika Kundi B, ambalo linaonekana kuwa na ushindani mkubwa baada ya Tanzania kukutana na mataifa yenye historia kubwa katika soka la wanawake duniani, Brazil, England na Canada.
Tanzania itaanza kampeni yake Septemba 5, 2026, kwa kucheza dhidi ya Brazil katika Uwanja wa Bielsko-Biala, kuanzia saa 11:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Baada ya mchezo huo, Tanzanite Queens itakutana na England Septemba 8 katika uwanja huo huo, ambapo mchezo huo utaanza saa 2:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi utakuwa dhidi ya Canada Septemba 11, 2026, katika Uwanja wa Arena Katowice, kuanzia saa 11:00 jioni.
Ratiba hiyo inawapa Tanzanite Queens mtihani mkubwa katika michuano hiyo, huku kila mchezo ukiwa muhimu katika harakati za kutafuta nafasi ya kufuzu hatua inayofuata.
Kocha Mkuu wa Tanzanite Queens, Bakari Shime, amesema ana imani na maandalizi ambayo timu hiyo imeyafanya tangu ilipoingia kambini Dar es Salaam.

Shime anaamini kikosi chake kina uwezo wa kufanya vizuri katika mashindano hayo na kufika hatua ya robo fainali, licha ya kukutana na wapinzani wenye uzoefu mkubwa katika soka la wanawake.
Kwa Tanzania, ushiriki wa Tanzanite Queens katika fainali hizo ni hatua muhimu katika historia ya soka la wanawake nchini, huku timu hiyo ikitarajiwa kupambana kuonyesha uwezo wake katika jukwaa kubwa la kimataifa.
Macho ya mashabiki wa Tanzania sasa yanaelekezwa Poland, ambako Tanzanite Queens itaanza safari yake ya kuandika historia katika Kombe la Dunia U-20.
Na Peter Jinni |GPL
