×

Furaha Kwa Wamiliki Wa Magari, Petroli Yashuka Kwa Shilingi 102 Na Dizeli Shilingi 101 Kila Lita

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei mpya za bidhaa za mafuta ya petroli nchini, huku bei ya juu ya rejareja ya petroli kwa Dar es Salaam ikifikia Shilingi 3,796 kwa lita kuanzia leo Jumatano ya Septemba 2,2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na EWURA, bei hizo zimezingatia mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia, ambalo limeendelea kukumbwa na misukosuko inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na vita vinavyoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.

EWURA imeeleza kuwa, katika mwezi Septemba 2026, bei za mafuta nchini zimeshuka kwa Shilingi 102 kwa lita ya petroli na Shilingi 101 kwa lita ya dizeli.

“Hii ni kutokana na hatua mbalimbali ambazo Serikali imezichukua ili kuwa na bei himilivu za mafuta hapa nchini.”

Kwa mujibu wa EWURA,kwa mwezi Septemba 2026, bei kikomo za rejareja za bidhaa za mafuta ya petroli katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ni kama ifuatavyo:

Bandari ya Dar es Salaam bei ya Petroli ni Shilingi 3,796 kwa lita, Dizeli ni Shilingi 3,877 kwa lita na Mafuta ya Taa ni Shilingi 3,713 kwa lita.

Katika Bandari ya Tanga, bei ya Petroli ni Shilingi 3,872 kwa lita, Dizeli ni Shilingi 3,953 kwa lita na Mafuta ya Taa ni Shilingi 3,789 kwa lita.

Aidha, katika Bandari ya Mtwara bei ya Petroli ni Shilingi 3,909 kwa lita, Dizeli ni Shilingi 3,990 kwa lita na Mafuta ya Taa ni Shilingi 3,825 kwa lita.

Vilevile, kwa mwezi Septemba 2026, bei kikomo za jumla za bidhaa za mafuta ya petroli katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ni kama ifuatavyo:

Katika Bandari ya Dar es Salaam bei ya Petroli ni Shilingi 3,649.09 kwa lita, Dizeli ni Shilingi 3,729.79 kwa lita na Mafuta ya Taa ni Shilingi 3,566.34 kwa lita.

Bandari ya Tanga bei ya Petroli ni Shilingi 3,670.26 kwa lita na Dizeli ni Shilingi 3,726.81 kwa lita, huku Bandari ya Mtwara bei ya Petroli ni Shilingi 3,653.33 kwa lita na Dizeli ni Shilingi 3,727.62 kwa lita.

Aidha, wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa rejareja na jumla wametakiwa kuuza mafuta kwa bei elekezi ambapo wale watakaokwenda kinyume watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Leave a Comment