
Msanii wa Bongo Fleva, Maua Sama, ametangaza kujifungua mtoto wa kike, akieleza furaha yake baada ya kuanza ukurasa mpya wa maisha akiwa mama.
Maua Sama ametoa taarifa hiyo kupitia mitandao yake ya kijamii, akimkaribisha duniani mtoto huyo na kueleza kuwa ujio wake umeleta furaha kubwa katika maisha yake.
“Welcome to the World Baby Girl. You guys, I have a MINI ME. It’s a Girl,” ameandika Maua Sama.
Msanii huyo pia amemshukuru Dkt. Lynn Moshi, ambaye amemtaja kuwa sehemu muhimu ya safari yake ya kujifungua, akieleza kuwa safari hiyo haikuwa rahisi kwake.
Maua Sama amesema kuna wakati alifikia hatua ya kuhisi huenda asingefanikiwa kujifungua salama, kabla ya kumshukuru Mungu kwa kumwezesha kumkaribisha mtoto wake duniani.

“Kuna wakati nilikuwa naona kabisa SITOBOI. Alhamdulillah,” amesema.
Taarifa za awali zilieleza kuwa Maua Sama alikuwa akitarajia mtoto wake wa kwanza, huku ujauzito wake ukiwa umeonekana hadharani katika kipindi cha mwisho cha safari yake ya ujauzito.
Maua Sama ni miongoni mwa wasanii wa kike wanaofanya vizuri katika muziki wa Bongo Fleva, akifahamika zaidi kupitia nyimbo zenye mchanganyiko wa R&B na Afropop. Ameendelea kuwa katika tasnia ya muziki kwa zaidi ya muongo mmoja na amewahi kutwaa tuzo mbalimbali za muziki nchini.
Mwaka 2022, alitoa EP yake “Cinema”, iliyoongeza nafasi yake katika muziki wa kizazi kipya nchini.
Kwa upande wake, Dkt. Lynn Moshi anatajwa kuwa mtaalamu wa Obstetrics and Gynecology, taaluma inayohusisha uzazi na afya ya mfumo wa uzazi wa wanawake.
Kwa sasa, Maua Sama ameanza rasmi safari yake mpya ya umama akiwa na mtoto wa kike ambaye amemuelezea kwa furaha kama “MINI ME.” 💗