
Hatua ya maswali ya dodoso (Cross-examination) kwa shahidi wa tatu wa upande wa utetezi katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, inaanza leo, Septemba 4, 2026.
Shahidi huyo, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Amani Golugwa, jana Septemba 3, 2026 alihitimisha kutoa ushahidi wake wa kumtetea Lissu mbele ya Mahakama.
Katika ushahidi wake, Golugwa ameiambia Mahakama kuwa haoni nia yoyote mbaya au ya uhaini kutoka kwa Lissu ambayo inaweza kuitishia Serikali.
Badala yake, amesema anachoona katika mashtaka yanayomkabili Lissu ni “nia ovu iliyotengenezwa makusudi” ili kuonesha uwepo wa kosa.
Kauli hiyo ilitolewa mbele ya Jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, baada ya Lissu kumuuliza Golugwa maoni yake iwapo ingeelezwa kuwa mshtakiwa ametengeneza nia ya uhaini kutokana na msimamo wake unaodaiwa kuashiria uasi.
Golugwa pia amesema kuwa, kwa mtazamo wake, Lissu hakuwa na nia yoyote ya kufanya uhaini kupitia maneno yaliyowasilishwa Mahakamani kama sehemu ya ushahidi wa Jamhuri dhidi yake.
Ikiwa hatua ya Cross-examination itakamilika leo, Lissu atapewa nafasi ya kumuuliza shahidi huyo maswali ya ufafanuzi (Re-examination), kabla Mahakama kutoa maelekezo mengine kuhusu mwenendo wa kesi hiyo.