×

Rais Samia Abuni Mpango wa Sifuri Tatu wa Mama Na Mtoto Afrika

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Ramani ya Utekelezaji ya Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Mtoto na Vijana kwa kipindi cha mwaka 2026–2030.

Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Septemba 9, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), sambamba na Kongamano la Pili la Kimataifa la Huduma za Afya ya Msingi.

Tukio hilo linafanyika kwa ushirikiano na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), likilenga kuweka afya na ustawi wa wanawake, watoto wachanga, watoto na vijana katika ajenda kuu ya maendeleo ya Afrika.

Ramani hiyo inalenga kutoa mwelekeo wa pamoja kwa nchi za Afrika katika kubadilisha ahadi na dhamira za kisiasa kuwa hatua madhubuti za kuimarisha huduma za afya.

Aidha, mpango huo unalenga kuongeza uwajibikaji, kuimarisha uwekezaji endelevu katika sekta ya afya na kuharakisha utekelezaji wa afua zinazoweza kuokoa maisha ya wanawake na watoto barani Afrika.

Katika ajenda hiyo, msisitizo umewekwa kwenye malengo ya “Sifuri Tatu”, ambayo ni sifuri ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na watoto wachanga, sifuri ya kujifungua katika mazingira yasiyo salama pamoja na rufaa zisizopata huduma stahiki za kitaalamu, na sifuri ya watoto ambao hawajapata chanjo.

Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Serikali, jamii, washirika wa maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi zinahimizwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa mikakati hiyo ili kuboresha huduma za afya kwa makundi hayo muhimu.

Dkt. Samia aliteuliwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto wakati wa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Februari 2026.

Kongamano hilo la Kimataifa la Huduma za Afya ya Msingi litakalofanyika Septemba 9 hadi 11, 2026, linatarajiwa kuwakutanisha watunga sera, viongozi wa sekta ya afya, wataalamu, watafiti, washirika wa maendeleo na wabunifu kutoka maeneo mbalimbali.

Washiriki hao watajadili mikakati ya kuimarisha Huduma za Afya ya Msingi na namna ya kuhakikisha huduma bora na zinazopatikana kwa wakati zinafika kwa wananchi barani Afrika.

Leave a Comment