×

Rais Samia Afanya Uteuzi wa Viongozi Sita Katika Nafasi Mbalimbali – Video

Dar es Salaam, Septemba 4, 2026 — Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi sita katika nafasi mbalimbali za umma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, baadhi ya uteuzi huo umejumuisha viongozi wapya kuchukua nafasi za waliomaliza muda wao.

Rais Samia amemteua Hamis Abdallah Mkunga kuwa Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, akichukua nafasi ya Mick Kiliba, ambaye amemaliza muda wake.

Katika uteuzi mwingine, Rais Samia amemteua Prof. Alfred Said Sife kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), akichukua nafasi ya Prof. William Anangisye, ambaye pia amemaliza muda wake.

Aidha, Jaji Mstaafu Wilfred Peter Dyansobera ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), akichukua nafasi ya Edriss Mavura, ambaye amemaliza muda wake.

Rais Samia pia amemteua Prof. John Modestus Lupala kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi.

Katika uteuzi mwingine, Rais amemteua Mhandisi Abdallah Mohamed Mkufunzi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Maji kwa kipindi cha pili.

Vilevile, Dkt. Henry Bethuel Mwanyika ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya TEHAMA, akichukua nafasi ya Prof. Leonard Mselle, ambaye amemaliza muda wake.

Taarifa hiyo imetolewa leo, Septemba 4, 2026, na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu.

Uteuzi huo unafanyika katika taasisi mbalimbali za umma zinazohusika na ajira, elimu, utatuzi wa migogoro ya kikazi, mipango ya matumizi ya ardhi, maji pamoja na TEHAMA.

 

Leave a Comment