
Dar es Salaam, Septemba 4, 2026 — Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ameliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta na kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria msanii wa muziki Godfrey Tumaini maarufu Dudu Baya, baada ya kushindwa kuitikia wito wa Wizara hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Katambi amesema Dudu Baya alitakiwa kufika katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi baada ya kutajwa katika tuhuma zinazohusiana na makosa ya jinai.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, msanii huyo aliitwa kwa mara ya pili, lakini bado hakufika katika ofisi za Wizara kama alivyotakiwa.

Katambi amesema Dudu Baya ameonekana kwenye mitandao ya kijamii akitoa kauli ambayo Waziri ameielezea kuwa ni ukaidi wa wito wa Serikali.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Katambi ameliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha msanii huyo anapatikana kokote aliko na kufikishwa mbele ya Jeshi hilo kwa ajili ya kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Agizo hilo linakuja wakati ambapo Dudu Baya amekuwa akizungumzia suala hilo kupitia mitandao ya kijamii, huku akieleza msimamo wake kuhusu wito alioupata kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Suala hilo limeendelea kuzua mjadala kwenye mitandao ya kijamii, huku wadau na mashabiki wa msanii huyo wakisubiri hatua zitakazofuata baada ya agizo hilo la Waziri.