
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Yusuph Masauni, ameongoza zoezi la usafi katika Soko la Buguruni jijini Dar es Salaam, huku akisisitiza kuwa agizo la kutumia siku ya Jumamosi kwa ajili ya usafi wa mazingira bado lipo na linapaswa kutekelezwa.
Masauni amesema usafi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja na kwamba mamlaka za Serikali zinapaswa kuhakikisha agizo hilo linasimamiwa na kutekelezwa katika maeneo yote.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Masauni amekumbusha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, wakati akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na akisimamia sekta ya mazingira, alitoa maelekezo ya siku ya Jumamosi kutumika kama siku maalumu ya usafi nchini.
Amesema pamoja na agizo hilo kutolewa, baadhi ya watu wamekuwa wakishindwa kulitekeleza kwa sababu mbalimbali.

“Leo nachukua nafasi hii kuwaambia kuwa maelekezo ya Makamu wa Rais Dk. Samia Hassan Suluhu, ambaye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenye nia njema ya kuhakikisha miji yote inakuwa safi, lile agizo halijafa,” amesema Masauni.
Amezitaka mamlaka zote za Serikali kuhakikisha zinasimamia utekelezaji wa agizo hilo na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi kila Jumamosi.
Masauni amesema usafi wa mazingira ni muhimu zaidi wakati wa msimu wa mvua, akieleza kuwa uchafu unaoweza kuziba mifumo ya maji unaweza kuongeza hatari ya mafuriko na kusababisha kuenea kwa magonjwa.

Ametaja kipindupindu na magonjwa mengine kuwa miongoni mwa madhara yanayoweza kujitokeza endapo mazingira yataachwa machafu.
Amesema kila mwananchi anapaswa kutimiza wajibu wake katika kuhakikisha eneo analoishi au kufanyia biashara linakuwa safi.
“Nimeona sokoni watu wana maduka madogomadogo. Kuna shida gani kuweka usafi kwenye eneo ulilopo? Viongozi wakisimamia hilo la usafi, maeneo yote yatakuwa safi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Masauni ameiomba Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupewa nguvu zaidi kisheria na kiutendaji ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Amesema NEMC inapaswa kuwa na uwezo wa kutosha katika kusimamia sheria za mazingira, kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kuchukua hatua dhidi ya watu wanaokiuka taratibu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema zoezi la usafi linaendelea na lengo ni kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa safi.
Mpogolo amesema Mkoa wa Dar es Salaam umeendelea kutekeleza maelekezo ya usafi kwa kusimamia usafi katika masoko, barabara na maeneo mbalimbali.
“Tumeendelea kusimamia agizo katika kila soko, kila barabara kuhakikisha usafi unaendelea kufanyika,” amesema Mpogolo.
Amesema juhudi za kuhakikisha mazingira yanakuwa safi zinapaswa kuendelea, huku akiwataka viongozi na wananchi kutokubali kuridhika bali kuongeza bidii katika kutekeleza majukumu yao.
Zoezi hilo la usafi katika Soko la Buguruni limekuja ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali na mamlaka za maeneo kuhakikisha usafi wa mazingira unasimamiwa kwa pamoja na wananchi wanashirikishwa katika kulinda mazingira yao.